Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 12, 2015

DRAW YA FAINALI ZA UEFA UERO 2016 IMEFANYIKA PARIS, UFARANSA

Na Paul Christian, Tabora. 

Draw ya makundi ya michuano ya Soka yenye hadhi ya pili kwa ukubwa na mvuto Duniani ya Kombe la bara la Ulaya (UEFA EURO 2016),inayotanguliwa na fainali za Kombe la Dunia imefanyika jana jioni katika jiji la Paris, Ufaransa. 

Fainali za michuano hiyo inafanyika katika ardhi ya Ufaransa na itaanza kutimua vumbi tarehe 10 ya mwezi Juni, 2016, kwa mechi ya ufunguzi kati ya wenyeji Ufaransa na timu isiyotabirika ya Romania katika uwanja wa Stade de France ambao pia utatumika kwa mechi ya fainali mnamo tarehe 10 Julai, 2016. 

Katika Draw hiyo Mabingwa watetezi wa kombe la Euro, Hispania walilolitwaa mwaka 2012 wakiongozwa na meneja Vicente Del Bosque watajaribu bahati yao kwa mara nyingine baada ya kufanya vibaya kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 ambapo walikuwa mabingwa watetezi, wako kundi D lenye timu nyingine za Jamhuri ya Czech, Uturuki na Krotia. 

Mabingwa wa kombe la Dunia katika fainali za mwaka 2014 nchini Brazil, Timu ya Ujerumani chini ya uongozi wa meneja wake Joachim Low wako kundi C pamoja na nchi za Ukraine,Poland na Ireland ya Kaskazini. 

Aidha Draw hiyo imeikutanisha Uingereza na ndugu zao Wales itakayoongozwa na Gareth Bale anayeichezea klabu ya Real Madrid ya Hispania na Aaron Ramsey anayeichezea Asernal ya Uingereza katika kundi B pamoja na nchi nyingine za Urusi na Slovakia. 

Wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2016 Ufaransa inayoongozwa na meneja Didier Deschamps iko katika kundi A ikiungana na nchi nyingine za Romania, Albania na Uswisi. 

Timu ya Ubelgiji iliyofika hatua ya robo fainali kwenye fainali za kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014 ikiwa chini ya uongozi wa meneja Marc Wilmots imepangwa kundi E pamoja na Italy, Jamhuri ya Ireland na Sweden.

Jumla ya timu 24 zilizofuzu fainali hizo za Euro 2016 zimepangwa katika makundi sita yenye timu nne kila moja. 

Makundi ya hayo ni kama ifuatavyo:- 

Kundi A: Ufaransa, Romania, Albania, Uswisi. 
Kundi B: Uingereza, Urusi, Wales, Slovakia. 
Kundi C: Ujerumani, Ukraine, Poland, Ireland ya Kaskazini. 
Kundi D: Hispania, Jamhuri ya Czech, Uturuki, Kroatia. 
Kundi E: Ubelgiji, Italia, Jamhuri ya Ireland, Sweden. 
Kundi F: Ureno, Iceland, Austria, Hungary.

No comments: