![]() |
Bwana Samson Amos akifafanua jambo |

Na Paul Christian, Tabora.
Viongozi wa serikali wameshauriwa kuwa makini
wakati wa kutoa matamko au kuchukua hatua za kiutendaji wakati huu wa kaulimbiu
ya hapa kazi tu.
Ushauri huo umetolewa na mshauri wa tiba mbadala
wa bidhaa za Tiens mjini Tabora Samson Amosi katika mahojiano maalum na
mwandishi wa Tabora Watch Blog.
Amesema kauli ya serikali ya hivi karibuni ya
kusitisha matangazo ya wataalam wa tiba mbadala kwenye vyombo vya habari pamoja
na kuweka masharti ya kuhariri matangazo hayo kabla ya kwenda hewani inapaswa
kutekelezwa kwa umakini ili kutenda haki.
Samson amesema, “kama lengo ni kudhibiti ubora wa
bidhaa, huduma au utaalamu wa tiba mbadala itakuwa vyema tukiona juhudi hizo katika
matangazo ya vileo, sigara na uzalishaji wa tumbaku bidhaa ambazo zinamadhara
ya wazi kwa afya za walaji.”
Amebainisha kuwa baadhi ya bidhaa zinazotumiwa
kwenye tiba mbadala zimetengenezwa kwa
virutubisho na madini kama chakula cha ziada kwa watu waliokosa na kusababisha
miili yao kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.
Samson amesema bidhaa hizo zimetengenezwa baada ya
kufanyiwa utafiti wa kina uliothibitisha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko
hata dawa zinazotumiwa hospitalini ambazo nyingi zinamadhara kwenye miili licha
ya kutibu.
Mshauri huyo wa tiba mbadala amefafanua kuwa watendaji wa serikali wasitekeleze majukumu
yao kwa kumfurahisha Rais John Pombe Magufuli
bali wafanye hivyo kwa kuwa ni wajibu wao wa kulinda na kutetea maslahi ya
taifa.
Samson amesema sekta ya afya inahitaji uwekezaji
wa maarifa na ufahamu wa hali ya juu katika ugunduzi wa dawa za asili zenye
uwezo wa kutibu magonjwa ambayo hayatibiki katika hospitali za mfumo rasmi.
Amefafanua kuwa taifa linapaswa kuwekeza kwenye
tafiti zitakazotoa majibu sahihi ya tiba za magonjwa sugu badala ya kubeza na
kukumbatia dawa zilizogunduliwa na wataalamu wa mataifa mengine .
Aidha amesema kuwa licha ya kutoa ushauri wa tiba
mbadala amekuwa akilipia leseni yake ya biashara shilingi 80,000/= , kodi ya
mapato shilingi 200,000/= pamoja na kodi ya pango shilingi 1,200,000/= kwa
mwaka hali, inayoonyesha uhalali katika shughuli anazozifanya.
Samson ameongeza kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa
TFDA kanda imeagiza kuanza kulipwa shilingi 60,000/= kwa mwaka jambo
linaloongeza mzigo mwingine kwa washauri wa tiba mbadala ambao wanatekeleza
majukumu yao kwa kamisheni.
Amesisitiza kuwa licha ya Tanzania kuwa na mimea
na vitu vingine vya asili wataalamu wake wameshindwa kushirikiana na kugundua
dawa, virutubisho au madini kupitia mimea hiyo
kwa lengo la kuzalisha bidhaa za kitanzania kama zilivyo nchi za Mashariki ya mbali.
No comments:
Post a Comment