Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 26, 2015

JESHI LA POLISI KALIUA LAWAMANI



Na Mwandishi Wetu,Kaliua
 
JESHI la polisi wilaya ya Kaliua mkoani Tabora limelalamikiwa na wananchi wa kijiji cha Mwahalaja, kata ya Igwisi wilayani humo kwa kuomba fedha za mafuta Tsh 600,000/= kila yanapotokea mauaji ya mwananchi.
 
Wakiongea kwenye kikao cha uchaguzi wa viongozi wa sungusungu wa kijiji cha hicho wananchi hao walisema wamechoshwa na tabia ya polisi kuwatoza kiasi hicho cha fedha kila yanapotokea mauaji ya ndugu zao.

Wakiongea kwenye mkutano huo wananchi hao walisema yalitokea mauaji ya Nassor Ally na Juma Mbogoni aliyeuawa Oktoba 7,2015 kwa shambulio la mapanga ndugu wa marehemu walitozwa Tsh 600,000/=  na polisi kama gharama ya mafuta.

Wananchi hao waliiomba serikali ya mkoa kuingilia kati kwani wamechoshwa na hali kuombwa fedha hiyo huku wakilalamikia pia kila wanapofanya makosa ya kawaida hutozwa hadi shilingi milioni nne.

 Machemba Ngeleja ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Mwahalaja alisema yeye alisingiziwa kosa  la kula njama za kumdhuru mtendaji wa kijiji cha hicho Shukuru Ngoma ambapo polisi walichukua magunia 20 ya mpunga na ng’ombe  tisa.

Ngosai Lutapia mkazi wa kijiji hicho alieleza kuwa alibambikiwa kesi ya bangi na kutozwa faini ya Tsh 120,000/=  na askari polisi wa wilaya hiyo ya Kaliua.

Afisa mtenda wa kijiji cha Mwahalaja Shukuru  Ngoma akiongea kwenye mkutano huo alisema ni kweli amekuwa akiwakamata watuhumiwa na kuwahifadhi ofisini kwake lakini  siku moja wananchi walivunja mlango na kumuua Juma Mbogoni na yeye aliwajulisha polisi na walipofika aliwakabidhi maiti hiyo.

Mtendaji huyo alisema baadhi ya watu walikamatwa na polisi katika tukio hilo nikasikia walitozwa fedha na kuachiwa huru lakini nashindwa kuthibitisha maana walikuwa wakipelekwa Kaliua huku wengine wakitoa fedha kwa kujificha.

Ngoma alisema kijiji chake kina kaya 455 na kwamba wakazi wake kwa sasa wanaishi kwa hofu kwani wengi wao wamefilisika kwa kuuza ng`ombe ili watoe fedha kwa polisi na kiwango kinachotozwa ni kati ya shilingi milioni moja hadi tano  kulingana na kosa analokutwa nalo.

Kuhusu kuanzisha upya jeshi la sungusungu Ngoma alisema wameamua kufanya hivyo kupunguza uhalifu kwani wananchi wamekuwa wakiishi kwa visasi vya ugoni na wizi wa mali za watu.

Kamanda wa polisi wilaya ya Kaliua (OCD)  M R Markuhi alipoulizwa juu ya malalamiko ya wananchi hao alisema hajui chochote wala hajapokea taarifa toka kwa mwananchi ambaye aliombwa Tsh 600,000/= ya mafuta na kuahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora (ACP) Khamis Seleman alisema hana taarifa hizo na kwamba wananchi wanapaswa kuwataja askari wanaohusika na udanganyifu huo.

Alisema kama kuna askari wamehusika atafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua lakini pia wananchi nao watoe ushirikiano kwani kiasi cha Tsh 600,000/=  kwa madai za  mafuta ni wizi.

No comments: