Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, December 30, 2015

HALMASHAURI YA WILAYA YA UYUI YAVUNJA MKATABA NA KAMPUNI YA SARAM


Na Halima Ikunji ,Tabora. 
Halmashauri ya wilaya ya Uyui mkoani Tabora imevunja mkataba wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje OPD katika hospitali ya wilaya hiyo kufuatia Mkandarasi kampuni ya SARAM kukiuka masharti ya mkataba huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hadija Makuwani amesema kampuni hiyo ya jijini Dar es Salaam imesitisha shughuli za ujenzi wa OPD hiyo iliyopo Isikizya makao makuu ya wilaya hiyo.

Amesema mkandarasi huyo amesimamisha shughuli za ujenzi kwa muda wa miezi 9 na hivyo kwenda kinyume na kifungu namba 62.2 cha mkataba huyo.
Hadija ameeleza kuwa mkandarasi huyo pia alikiuka vifungu namba 10.1 na 10.2 vya mkataba huo kwa kumtumia mtaalamu ambaye hatambuliki kwenye mkataba huo.

Mkurugenzi huyo mtendaji ametaja sababu nyingine zilizosababisha kuvunjwa kwa mkataba huo ni mkandarasi huyo kushindwa kuhudhuria vikao vya kazi vilivyoitishwa na msimamizi wa mradi huo jambo ambalo ni kinyume na kifungu namba 35.2 cha mkataba huo.

Hadija amebainisha kuwa hatua za kuvunja mkataba huo zimezingatia kifungu cha 62.1 ambacho kinamtaka mwajiri au mkandarasi kuvunja mkataba endapo mmoja kati yao atashindwa kutimiza masharti ya mkataba huo.

Aidha amefanunua kuwa wakati mkataba unavunjwa mkandarasi huyo alikuwa ametekeleza kazi yenye thamani ya sh. 138,109,468.86 na madai
anayostahili ni sh. 3,564,245.59 kama malipo ya kazi.

Hadija amekiri kuwa  kiasi cha sh.5,650,157.95 kama malipo ya kinga iliyokuwa imekatwa kwenye hati alizokwishalipwa na kuongeza kuwa malipo ya fedha hiyo atalipwa baada ya tathmini ya mwisho.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa gharama za mkataba wa kazi hiyo ilikuwa sh 299,654,364.60 huku nyongeza ikiwa ni sh 15,257,200.00 jambo linalofanya gharama ya mradi wote kuwa kiasi cha sh 314,911,564.60.

“mkataba huo umevunjwa rasmi tarehe 22 mwezi huu baada ya kujiridhisha pasipo shaka kuwa mkandarasi ameshindwa kutimiza matakwa ya kisheria ya mkataba wake’, alisema Mkurugenzi.

Hivi karibuni Halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ilisitisha mkataba na kampuni hiyo ya ujenzi kwa madai ya kukiuka mkataba wa ujenzi wa ofisi ya mkurugenzi, jengo la wagonjwa wa nje OPD, nyumba za watumishi, jengo la maonesho katika eneo la Ipuli mjini Tabora.

No comments: