Na Paul Christian, Tabora
Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete
inakabiliwa na upungufu wa damu salama hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa
wanaohitaji huduma hiyo.
Akizungumzia hali hiyo meneja wa maabara ya
hospitali hiyo Abdallah Haruna alisema mahitaji
halisi ni wastani wa Unit 15 hadi 20 kwa siku lakini kwa sasa wanapokea
wastani wa Unit 5 kwa siku kutoka Benki ya damu salama kanda ya Magharibi.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiwasababisha kugawanya
mara mbili damu salama iliyomo kwenye
mfuko mmoja wenye ujazo wa mililita 500 kwa lengo la kuwahudumia wagonjwa
wawili kwa wakati mmoja.
Abdalla amebainisha kuwa njia nyingine
wanayoitumia kukabiliana na hali hiyo ni ndugu wa wagonjwa kujaza fomu maalumu na
kujitolea damu.
Alibainisha kuwa hali huwa mbaya zaidi pale
wanapokuwa na mgonjwa anayehitaji kuongezewa damu kutoka katika kundi O hasi
ambalo linawatu wachache sana.
Meneja huyo wa maabara alisema tabia ya kundi la
damu O hasi linaweza kumuongezea mtu yoyote lakini mtu mwenye kundi O hasi
akihitaji damu ni lazima aongezewe na mtu mwenye kundi kama hilo tu.
Afisa tawala na utumishi wa Mpango wa Damu Salama
kanda ya Magharibi Ludovick Mlay alikiri kuwepo kwa upungufu wa damu salama katika
hospitali ya Kitete kutokana na kushuka kwa uchangiaji damu kwenye Mpango.
Alisema sababu mojawapo ya kushuka kwa uchangiaji huo
ni kukosekana maandalizi ya kutosha ya kuuendesha Mpango wa damu salama mara
baada ya ufadhili wa Marekani kufikia ukomo mwezi Mei mwaka huu.
Mlay alibainisha kuwa serikali iliziagiza halmashauri za wilaya nchini
kubeba jukumu la kukusanya damu kutoka kwa wananchi na kisha kuipeleka benki ya
damu kwa ajili ya vipimo ili kubaini vimelea vya homa ya Ini B na C,Kaswende na
Virusi vya UKIMWI.
Afisa tawala huyo alieleza kuwa halmashauri nyingi
katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida na Katavi hazijaanza kutekeleza zoezi hilo kwa madai ya kutokuwa
na fedha.
Alisema, “kutokana na utaratibu wa sasa
halmashauri zinatakiwa kukusanya damu asilimia 80 ya mahitaji yote huku
asilimia 20 inayobaki inakusanywa na Benki ya damu Salama.”
Mlay alibainisha kuwa benki ya damu salama yenye
makao yake mjini Tabora inatakiwa kukusanya unit 500 kwa mwezi sawa na wastani
wa Unit 18 kwa siku.
Aidha alitaja sababu nyingine zinazozorotesha zoezi la uchangiaji damu kuwa ni uuzwaji wa
damu salama kwenye hospitali na vituo vya afya badala ya kutolewa bure pamoja
na urasimu wakati wa kutoa huduma.
Mlay alieleza kuwa kundi la wanafunzi wa sekondari
na vyuo ndilo linalotegemewa sana kuchangia damu na kwamba inapofika miezi ya likizo
makusanyo ya damu hushuka.
Hata hivyo alionesha kuwa na matumaini kuwa
utaratibu mpya wa ukusanyaji damu kupitia halmashauri utaongeza makusanyo na
kuondoa tatizo la upungufu wa damu Salama.
Mahitaji ya
damu Salama kanda ya Magharibi ni wastani wa unit 67,000 kwa mwaka ambayo zaidi
inahitajika kuokoa maisha ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, akinamama
wajawazito, operesheni na wagonjwa wa ajali.
Benki ya damu salama kanda ya Magharibi ilianza
shughuli zake mwaka 2007 na inahudumia mikoa ya Tabora,Kigoma,Katavi na
Singida.
No comments:
Post a Comment