Na Hastin Liumba,Kaliua
WAKAZI wa kata ya Zugimlole wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wameshangazwa na hatua ya maofisa wa maliasili kuwazuia kufanya shughuli za kilimo katika maeneo yanayodaiwa ni sehemu ya hifadhi ya Mpanda Forest na Sawima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa Kitongoji cha Kanyanya, kijiji cha Imbulisiasi pamoja na kitongoji cha Iga kijiji cha Uyumbu walisema hatua hiyo imeathiri uzalishaji wa chakula na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kukumbwa na njaa.
Wakazi hao walibainisha mazao ya chakula waliyolima katika maeneo hayo kuwa ni mahindi na mpunga kabla ya kutakiwa kusitisha shughuli hizo tarehe 12 mwezi huu.
Aidha walieleza kuwa maofisa wa
maliasili waliwanyang’anya zana zao za kilimo jambo linalowafanya washindwe kufanya
shughuli za kilimo kwenye maeneo mengine.
Mmoja wa wakazi hao Peter Luhimba
alisema serikali imeshindwa kuainisha mipaka ya hifadhi hizo jambo
linalowachanganya na kushindwa kuelewa mipaka halisi ni ipi ili waiheshimu
tofauti na ilivyosasa.
Sai Juma alibainisha kuwa wao kama
wananchi ni sehemu ya uhifadhi wa hifadhi hizo hivyo wanapaswa kuijua mipaka
pamoja na kushirikishwa ipasavyo katika ulinzi badala ya kuchukuliwa kama
waharibifu.
Naye Leonard Charles alieleza kwamba
hali ya kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kwenye hifadhi hizo kunawafanya baadhi ya
watumishi wa maliasili kuwaonea na kuwanyanyasa wananchi kwa lengo la
kujinufaisha.
Kwa kauli moja wakazi hao wameiomba
serikali kuangalia uwezekano wa kuwaruhusu wahudumie mazao yao hadi yatakapo komaa
na kuvunwa ambapo watatafuta maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo.
wameztaja zana zao za kilimo zilizochukuliwa na maafisa hao wa maliasili kuwa ni pamoja na majembe ya mkono, matrekta na ng’ombe wanao kokota majembe ya kilimo.
Diwani wa kata ya Zugimlole Balikeka Ramadhan alipohojiwa kuhusu suala hilo alisema wananchi wake sasa hawalimi baada ya kunyang’anywa zana za kilimo.
Diwani huyo alisikitishwa na maofisa hao wa maliasili kufika katika maeneo hayo yanayodaiwa yako ndani ya hifadhi bila kushirikiana na uongozi wa kata hiyo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Athuman Kihamia alisema
zoezi hilo halikufanywa na maofisa wa ofisi yake bali lilifanywa na wakala wa misitu nchini TSF.
Alipohojiwa Mkuu wa wilaya Kaliua
Hadijah Nyembo alisema naye alisema zoezi hilo la kuwahamisha wananchi
wanaodaiwa kuwa ndani ya hifadhi wahusika ni Maliasili hivyo wakiulizwa
watakuwa na majibu ya msingi.
Meneja misitu wa wilaya ya Kaliua John Madohora alisema wananchi hao
ni kweli wameingia na kuvuka mipaka ya hifadhi na wanaendesha kilimo.
Madohora alisema tumekuwa tukiwaondoa kisheria na kwamba tatizo kubwa lipo kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwani wamekuwa wakichukua fedha na kuuza maeneo ya hifadhi.
Aliyataja maeneo ambayo wananchi wamevamia ni Mpanda Line kwenye maeneo ya Kangeme, Lumbe, Usinge, Ukumbisiganga na Kakole na kwamba zipo taratibu za kuangalia mipaka na kwaleza wazi kuwa wako kwenye hifadhi.
Alisema
alama za mipaka zipo na zinaonekana bayana na kumekuwa na jitihada za kufyeka
nyasi ili ziweze kuonekana kwa uwazi.Meneja misitu wa wilaya ya Kaliua John Madohora alisema wananchi hao
ni kweli wameingia na kuvuka mipaka ya hifadhi na wanaendesha kilimo.
Madohora alisema tumekuwa tukiwaondoa kisheria na kwamba tatizo kubwa lipo kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwani wamekuwa wakichukua fedha na kuuza maeneo ya hifadhi.
Aliyataja maeneo ambayo wananchi wamevamia ni Mpanda Line kwenye maeneo ya Kangeme, Lumbe, Usinge, Ukumbisiganga na Kakole na kwamba zipo taratibu za kuangalia mipaka na kwaleza wazi kuwa wako kwenye hifadhi.
Madohora alisema wanasiasa wanaingilia kati kuwatetea wananchi waendelee kukaa kwenye hifadhi lakini mamlaka inachukua hatua hizo kunusuru misitu.