Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Friday, February 26, 2016

MAHAKAMA KUU KANDA YA TABORA YATUPILIA MBALI SHAURI LA KUPINGA MATOKEO YA UBUNGE JIMBO LA TABORA MJINI


Na, Thomas Murugwa, Tabora.
Mahakama kuu kanda ya Tabora imetupilia mbali shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa Ubunge wa jimbo la Tabora mjini lililofunguliwa na wanachama wanne wa Chama Cha Wananchi CUF na kuwataka walipe gharama  walizoingia wadaiwa.

Uamuzi huo umefikiwa na jaji Leila Mgonya baada ya kukubaliana na pingamizi la mawakili wa  wadaiwa ambao ni mbunge wa jimbo, Msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria mkuu wa serikali kwamba walalamikaji hawakuwa na mamlaka na pia hawakuonyesha haki yao iliyovunjwa wakati wa zoezi la uchaguzi.

Jaji Mgonya katika uamuzi wake aliousoma kwa saa mbili amesema kuwa anakubaliana kwamba haki yao ya kuleta shauri hilo inatokana na kifungu namba 111 (1) cha Sheria ya uchaguzi  lakini hawakuwa na mamlaka kisheria.

“kutokana na sheria za nchi ili mtu awe na mamlaka ya kufungua shauri la kupinga matokeo kama siyo mgombea inabidi aeleze jinsi gani haki yake ilivyovunjwa na pia alivyoumizwa”  amesema jaji Mgonya.

Katika maamuzi hayo, jaji Mgonya amewataka walalamikaji ambao ni wananchama wanne wa  CUF walipe gharama walizotumia wajibu maombi wakati wa uendeshaji wa shauri hilo tangu lilipofunguliwa tarehe 25 Novemba 2015 hadi  lilipomalizika.

Wanachama hao wanne wa CUf ambao ni Jumanne Mtunda ,Johari Kasanga, Shaban Mussa na Thomas Ayengo kupitia kwa wakili wao Job Kerario waliiomba mahakama itengue matokeo ya uchaguzi uliompa ubunge Emanuel Mwakasaka wa CCM kwa madai haukuwa huru na wa haki.

Upande wa wajibu maombi ulikuwa unawakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Juma Masanja pamoja na Kamaliza Kayaga aliyekuwa anamwakilisha mbunge wa jimbo hilo,Emmanuel Mwakasaka.


No comments: