Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Thursday, February 11, 2016

HALMASHAURI YA WILAYA YA SIKONGE YAPITISHA BAJETI YA MAENDELEO YA BILIONI 23.9


Na Allan Ntana, Sikonge

HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imepitisha bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni 23.859 itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Akisoma taarifa ya mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya wilaya hiyo kwa mwaka 2016/2017 kwenye kikao cha baraza la madiwani Afisa Mipango wa halmashauri hiyo Ernest Kahabi amebainisha kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele muhimu vya miradi ya maendeleo.

Amesema halmashauri hiyo imeomba kuidhinishiwa kiasi hicho cha shilingi bilioni 23.859 ikiwa makisio ya mapato na matumizi ya kawaida ni kiasi cha shilingi bilioni 18.818 ambazo shiling bilioni 16.612 ni matumizi ya mishahara na shilingi bililioni 2.205 ni matumizi mengineyo.   

Amebainisha kuwa miradi ya maendeleo pekee imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 5.041 ambapo fedha za ndani ni shilingi bilioni 3.636 (ruzuku toka Serikali Kuu ikiwa ni sh bil 2.126 na mapato ya ndani ya halmashauri sh bil 1.559) na fedha za nje ni shilingi bilioni 1.355 ( kutoka Serikali Kuu ikiwa ni shilingi milioni.545.887 na asasi zisizo za kiserikali shilingi milioni 810.110).

Kahabi amesema mapendekezo ya bajeti hiyo yatatokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo ruzuku toka Serikali Kuu kiasi cha shilingi bilioni 20.455 ambapo matumizi ya mishahara ni sh bil 16.492 na matumizi mengineyo ni shilingi bilioni 1.290 huku miradi ya maendeleo ikitengewa shilingi bilioni 2.636.

Mapato yatokanayo na michango ya wahisani ambao ni asasi zisizo za kiserikali alisema wanatarajia kupata kiasi cha sh mil. 810 (milioni 604 kutoka EQUIP UK na mililioni 205 kutoka EGPAF).

Afisa Mipango huyo ameongeza kuwa halmashauri hiyo inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi bililioni 2.594 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani ambapo matumizi ya mishahara itakuwa shilingi milioni 120 na matumizi mengineyo shilingi milioni 915 huku miradi ya maendeleo ikitengewa shilingi bilioni 1.559 sawa na asilima 60 ya mapato yote ya ndani.

Akielezea mapendekezo ya bajeti hiyo, iliyowasilishwa na Afisa Mipango kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Philemon Magesa, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Peter Nzalalila aliomba madiwani waiunge mkono kwa kuwa imegusa maeneo yote ya kimaendeleo kama walivyopendekeza.

Ametaja baadhi ya vipaumbele vya bajeti hiyo kuwa ni kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Mazinge ili kukifanya kuwa hospitali ya wilaya, kuimarisha miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari kwa kujenga vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.

Kuboresha huduma ya maji safi na salama ikiwemo kukamilisha miradi ya maji Kipili na bwawa la maji Igumila lililopo katika kata ya Kitunda ikiwemo ujenzi wa Soko Kuu na stendi mpya, kuanzisha kidato cha tano katika shule ya sekondari Kamagi na kuendeleza michezo kwa vijana.







No comments: