Na Paul Christian, Tabora
Wananchi wa kijiji cha Ishihimulwa kata ya Bukumbi
wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa mara nyingine wameikataa taarifa ya mapato na
matumizi ya upangaji wa mnara wa simu za mkononi Airtel uliopo kwenye eneo la shule
ya msingi Ishihimulwa kijijini humo.
Kwa kauli moja wananchi hao kupitia mkutano mkuu wa
pili wa kijiji hicho walimzuia mtendaji wa kijiji hicho Jiji Numbu kuendelea
kuisoma taarifa kuhusu mradi huo wa mnara wa simu kwa kuwa haikuakisi hali
halisi ya mapato yanayolipwa na kampuni ya Airtel kwa uongozi wa shule hiyo.
Wananchi hao wamemshutumu mwalimu mkuu wa shule
hiyo kutumia kwa manufaa yake binafsi fedha zinazotolewa kama malipo ya pango
na kampuni inayomiliki mnara huo.
Msimamo huo wa wananchi umetolewa baada ya mara ya
kwanza kuikataa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi huo wa mnara wa simu
iliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa kijiji uliofanyika tarehe 18 mwezi uliopita
na kuonyesha kuwa kwa mwaka wa 2015 mnara huo uliingiza mapato ya shilingi
90,000/= badala ya shilingi 1,600,000/= kwa mwaka kama ilivyoainishwa kwenye
mkataba.
Aidha Katika mkutano huo wa pili wananchi hao
waliikataa serikali ya kijiji inayoongozwa na Edward Daniel kwa kukaidi maagizo
waliyopewa na diwani wa kata ya Bukumbi John Majala ya kuivunja kamati ya shule
hiyo pamoja na kuwasilisha kwa wananchi hati ya benki inayoonesha mwenendo wa
fedha wa akaunti ya shule husika.
Wananchi hao wamehoji mapato ya mnara huo wa simu ili waweze kujenga choo cha wanafunzi wa shule
hiyo ambao kwa sasa wanahangaika kwa kujihifadhi.
Aidha wamemshutumu mwalimu mkuu wa shule hiyo ya
msingi kushindwa kuhudhuria mikutano mikuu ya kijiji kwa madai ya kuwa na
majukumu ya kikazi hali inayoashiria kuna jambo analolificha kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment