Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Tuesday, February 9, 2016

WATENDAJI WAAGIZWA KUWASAKA WAZAZI WASIOPELEKA SHULE WATOTO WALIOFAULU DARASA LA SABA



SULEIMAN KUMCHAYA

Na Allan Ntana, Tabora


WAZAZI wote wenye watoto waliofaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanajiunga kidato cha kwanza vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Tabora Suleiman Kumchaya
katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya
Tabora kilichofayika Juma katika ukumbi wa manispaa hiyo.

Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kutohimiza
watoto wao kwenda shule au kutowapeleka watoto waliofaulu kuingia
kidato cha kwanza kwa kutoona umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

Amewataka Watendaji wa kata zote 29 zilizoko katika manispaa hiyo
kuhakikisha wanawasaka wazazi wote ambao watoto wao hawajaripoti
shuleni hadi sasa ili hatua kali zichukuliwe mara moja.

‘Naagiza kila Mtendaji wa kata afuatilie na ahakikishe watoto wote
waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wamejiunga, tembeeni usiku
na mchana ili kubaini mzazi asiyetekeleza agizo hilo.’ amesisitiza.

Ameongeza kuwa watoto wote waliofikia umri wa kuanza shule wanapaswa kupelekwa kuanza elimu ya awali na kisha darasa la kwanza na kuendelea kwani elimu hiyo sasa inatolewa bure, hakuna sababu ya kumnyima mtoto haki yake.

Aidha aliwataka watendaji hao kuzunguka katika mitaa yao yote ili
kuhakikisha zoezi la usafi linatekelezwa na wananchi katika kata zao
kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kwa wale watakaokaidi maelekezo
hayo wachukuliwe hatua mara moja.

Akizungumzia suala la madawati kwa kila shule, amemtaka Mkurugenzi
Mtendaji wa Manispaa hiyo Sipola Liana kushirikiana kwa karibu na watendaji wake wote pamoja na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha kila
shule inakuwa na madawati ya kutosha kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

‘Tumeagizwa mpaka kufika mwezi Juni asiwepo mtoto hata mmoja wa kukaa chini sakafuni, hili linamhusu kila mmoja wetu kuanzia mkurugenzi,
madiwani, watendaji na wananchi kwa ujumla, naomba sana tushikamane
katika hili.’ Amesema mkuu huyo wa wilaya.

No comments: