Na Paul Christian.
Katika kipindi cha Maswali na Majibu leo Bungeni
mjini Dodoma, mbunge wa Urambo Mheshimiwa Magret Simwanza Sitta ameuliza swali la
msingi lifuatalo.
Mfumo wa sasa wa kuwahudumia
wakulima wa zao la Tumbaku wa wilaya ya Urambo na mkoa wa Tabora kwa ujumla
unamapungufu mengi unaowaletea wakulima usumbufu kama vile bei ya pembejeo kuwa
kubwa kutokana na kuagizwa nje, riba kubwa za benki, masoko ya Tumbaku kutokuwa
na uhakika na hatimaye kusababisha kushuka thamani, Je ni kwa nini hasara
inayotokana na matatizo hayo ibebwe na mkulima peke yake?
Akijibu swali hilo la Msingi Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha amesema, “Naibu
spika, serikali inakubaliana na mheshimiwa mbunge yapo maeneo mbalimbali
yanayomkosesha mkulima mapato, maeneo hayo ni pamoja na mfumo wa usambazaji
pembejeo uliokuwa na mianya mingi unaosababisha madeni hewa, baadhi ya viongozi
wa vyama kukopa fedha nyingi kupita uwezo wa vyama kuzalisha Tumbaku na
kadhalika.
“Kwa sasa serikali Imebadili
mfumo huo na kuelekeza wagavi wa pembejeo hizo kuzifikisha moja kwa moja kwenye
vyama vya msingi tofauti na utaratibu wa awali wa kupitisha pembejeo kwenye
vyama vikuu.”
“Aidha ili kuwa na uhakika wa soko kilimo
cha Tumbaku nchini uendeshwa kwa mkataba kati
ya wanunuzi na wakulima, hivi sasa bei upangwa kabla ya msimu kilimo
kuanza ili mkulima ajue bei na kiasi ambacho mkulima anatakiwa kuzalisha.”
“Tatizo la soko na bei mara nyingi
uwakumba wale wakulima wanaozalisha tumbaku bila kuwa na mikataba ambapo
ujikuta tumbaku yao ikikosa soko au wakipewa bei ya chini.”
“Mheshimiwa Naibu Spika, serikali
imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zinazomkabili mkulima wa
Tumbaku, hatua hizo ni pamoja na kuboresha mfumo wa upangaji wa bei ya Tumbaku ambapo
wakulima hupendekeza bei yenye tija kwao na kuiwasilisha kwa wanunuzi kupitia
vikao vya halmashauri ya Tumbaku yaani Tobacco Council, bei hiyo hujadiliwa na
hatimaye kufikia muafaka.”
“Mfumo huu wa upangaji wa bei
umeanza kutumika rasmi msimu wa 2015/2016 sanjari na maboresho ya mfumo huu
serikali inaendelea na jitihada za kuongeza wanunuzi wa tumbaku kutoka China
ili kuongeza ushindani kumuwezesha mkulima kupata bei nzuri.”
“Aidha serikali itapitia tozo za
pembejeo zinazoingia nchini na kuangalia uwezekano wa kuziondoa ili kumpunguzia
mkulima gharama za uzalishaji.”
Mheshimiwa Magret
Simwanza Sitta ameuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) “Mheshimiwa Naibu Spika Waziri amekiri kwamba
mfumo uliopo unamatatizo katika kumuhudumia mkulima, lakini serikali inashiriki
kikamilifu katika kupanga bei katika mfumo mzima, sasa kwa kuwa serikali
inashiriki kwa kupitia wakala wake Bodi au Council, je serikali haioni kwamba
inawajibika kubeba sehemu ya hasara anayopata mkulima?”
b) “Kwa kiasi gani mmefaulu kupata wanunuzi zaidi
kutoka China ili soko liwe la haraka wakulima wanufaike?”
Akijibu maswali hayo ya nyongeza Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole amesema, “Tobacco
Council au halmashauri ya Tumbaku inawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya Tumbaku,
serikali yenyewe haihusiki moja kwa moja katika kupanga bei lakini imeweka utaratibu
ambao wadau wenyewe wanaweza kukaa kukutana kwa uhuru wao na kupanga bei hata
hivyo serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba bei za tumbaku
zinaendelea kuwa nzuri.”
“Tunafahamu kwamba kuanzia mwaka 2013 Bunge hili
lilipitisha Sheria mpya ya vyama vya Ushirika, utaratibu mpya wa vyama vya Ushirika ni utaratibu ambao pamoja na mambo mengine unawaruhusu wakulima wa
mazao mbalimbali kuendesha shughuli zao kwa kuwa na uhuru zaidi, lakini vile
vile mpango ule umeunda Tume ya Ushirika ambayo inakuwa karibu na vyama vya
Ushirika ili kuweza kuondoa kero zilizopo tunafikiri utaratibu huu unaleta ufanisi
zaidi katika kilimo cha Tumbaku na mazao mengine ikiwa ni pamoja na kusaidia
suala la bei.”
“Lakini nitumie fursa hii kuwaeleza
waheshimiwa wabunge pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye sekta ndogo ya
Tumbaku, tunafikiri sekta ndogo ya Tumbaku ni eneo ambalo limeanza kuonyesha
mifano ya kufanikiwa hii ni kwa sababu ndio sekta ndogo ya pekee ambayo mkulima
anakuwa na uhakika wa kuuza zao lake tokea siku ya kwanza anapoanza kuweka
mbegu shambani kwa sababu ni kilimo cha mkataba.”
“Kwa hiyo tukiondoa changamoto
zilizopo tunafikiri ni eneo ambalo bado inawezekana kupata mafanikio makubwa lakini vile vile
tungependa kutumia usahihi kuwaeleza wakulima kuwafahamisha kwamba kufanikiwa
kutumia kilimo cha mkataba unaweza kusaidia tu kama kila mtu ataheshimu
mkataba.”
“Kwa mfano mwaka huu tayari wakulima
wanafahamu inatakiwa wazalishe tumbaku kiasi gani, tunaomba wale ambao hawako
kwenye mkataba wasizalishe tumbaku kwa sababu ukizalisha hautapata mnunuzi.”
Akijibu Kipengele (b) cha swali la nyongeza Naibu
Waziri huyo amesema, “mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali inajitahidi kuongea na wafanyabiashara kutoka China, tumefika hatua
nzuri sana kinachobakia sasa ni wao kumaliza taratibu za nchini kwao ili nao
waweze kuingia kwenye mfumo rasmi wa kununua Tumbaku ili kuondoa ukiritimba
ambao mpaka sasa hivi nchi nzima kampuni zinazonunua Tumbaku ni nne tu.”
“Kwa hiyo tunafikiri kwamba kampuni
zikiwa nyingi maana yake tutaondo Monopoly na hivyo bei itakuwa nzuri,
Nashukuru.”
No comments:
Post a Comment