Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, February 1, 2016

WANAFUNZI 700 WATUMIA VYUMBA VIWILI VYA MADARASA



WAZIRI WA ELIMU,SAYANSI,TEKNOLOJIA NA UFUNDI PROF. JOYCE NDALICHAKO

NA Lucas Raphael, Kaliua. 

Wanafunzi wapatao 700 wanakaa chini katika shule ya msingi Mtapenda iliyopo Kata ya Ufukutwa wilayani Kaliua  mkoani Tabora kutokana na kukosefu wa madawati.

Licha ya ukosefu  huo wa madawati shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingine ikiwemo ukosefu wa vyoo vya wanafunzi, upungufu wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na walimu  kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 40 kwa siku.

Akizungumzia suala hilo diwani wa kata ya Ufukutwa Abdallah Hemeda amesema  wanafunzi wa shule hiyo kwa sasa wanatumia choo chenye matundu manne ambacho kilikuwa cha walimu.
Amebainisha kuwa hali hiyo imewafanya walimu wa shule hiyo kutumia choo kimoja kilichopo kwenye nyumba moja ya mwalimu.

Diwani huyo ameiambia kamati ya Fedha na Mipango ya halmashauri ya wilaya ya Kaliua kuwa shule hiyo ina vyumba viwili vya  madarasa na chumba kimoja kati ya hivyo hakijakamilika ujenzi wake.
Abdallah amefafanua kutokana na hali hiyo wanafunzi 700 wanalazimika kuvitumia vyumba hivyo vya madarasa pamoja na kusomea chini ya miti ili kukidhi mahitaji.
Amebainisha kuwa hali ya kufundisha na kujifunza huwa ngumu zaidi  wakati wa kipindi hiki cha mvua ambapo wanafunzi wote ulazimika kujihifadhi kwenye vyumba hivyo vya madara huku walimu wakijihifadhi kwenye nyumba ya mwalimu.
Ameongeza kuwa shule hiyo inakabiliwa na mazingira magumu yanayowafanya  walimu wake kuishi mjini na kulazimika kutembea zaidi ya kilomita 40  kila siku.

Aidha diwani huyo amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa kuifanya shule hiyo kuongoza kitaaluma kati ya shule za msingi zilizopo kwenye kata hiyo licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo,Godfrey Alex ameitaka serikali kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na miundombinu mingine  kulingana na mahitaji ya shule.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kaliua Haruna Kasele amesikitishwa na hali hiyo na kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha anajenga vyumba vya madarasa ili kuondoa tatizo la msongamano na kusomea chini ya miti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Athuman Kihamia amesema agizo la mwenyekiti litaanza kutekelezwa ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili hule hiyo.

Amesema shule hiyo ni miongoni mwa zile ambazo hazikuwa katika utaratibu rasmi wa serikali kutokana na kujengwa na jamii ya wafugaji ambao wanahamahama.

Mkurugenzi huyo amekiri kuanza kuzisaidia shule kama hizo ambazo ziko kwenye mazingira magumu ya kujifunzia na kufundishia.


No comments: