Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, February 17, 2016

WAFANYABIASHARA WAMEKWEPA KODI, WANALIPA MISHAHARA KIDUCHU WAFANYAKAZI.

Na Paul Christian, Tabora.

DKT. JOHN P. MAGUFULI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akihimiza wafanyabiashara kufanya biashara halali na kulipa kodi sahihi na kwa wakati.

Hatua hiyo inalengo la kuongeza mapato ya serikali ili iweze kutimiza wajibu wake wa kutoa huduma za kijamii, kugharamia miradi ya maendeleo pamoja na uendeshaji wa serikali.

Rais huyo wa awamu ya Tano ameonyesha nia ya dhati ya kubana matumizi ya serikali,kuziba mianya ya ukwepaji kodi,kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka na kuifanya mifumo ya umma kufanya kazi yake ipasavyo.

Uchunguzi umebaini kuwa nia njema ya Rais Magufuli ya kuleta uwiano wa kipato cha mwananchi wa kawaida na ukuaji  wa uchumi wa nchi sanjari na kupunguza pengo la kipato kati ya matajiri na masikini haiwezi kufanyikiwa pasipo kuwawezesha wananchi kuwa sehemu ya  mabadiliko husika.

Kwa upande wa wafanyabiashara ambao wanawajibika kulipa kodi halali kwa serikali, ndio waajiri wakubwa wa Watanzania wenye elimu ya chini,kati na hata elimu ya juu.

Kwa miaka mingi, wengi wa wafanyabiashara hao licha ya kujihusisha na vitendo vya kuikosesha serikali mapato kwa kutokulipa kodi sahihi, wamekuwa wakilipa mishahara duni wafanyakazi wao.

Kwa mantiki hiyo dhamira ya Rais Magufuli haiwezi kufanikiwa endapo wafanyabiashara hao watalipa kodi stahiki kwa serikali,  huku wakiendelea kulipa mishahara duni inayodhalilisha utu wa mtanzania.

Tanzania imekuwa na udhaifu mkubwa wa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa kutimiza majukumu kwa maslahi ya umma na badala yake maslahi ya wachache yamekuwa yakipewa nafasi hata kwa kupindisha Sheria.

Serikali ya awamu ya Nne ilifanya jitihada za majadiliano, uundaji wa miundombinu na usimamizi wa kisekta kwa lengo la kuboresha mishahara ya wafanyakazi katika sekta binafsi.

Lakini hatua hiyo mara zote imeshindwa kufua dafu kwa wafanyabiashara matajiri ambao wameonyesha kuwa na sauti zaidi ya Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.

Ushahidi wa kiburi, jeuri na dharau ya wafanyabiashara hao umejidhihirisha kwa kugomea kuwapa mikataba wafanyakazi wao kwa madai na visingizio vilivyo nje ya Sheria husika na serikali ikawa kimya.

Dkt. Magufuli atakapo kusanya kodi yake na kuacha wafanyakazi wake wakiwa na usalama mdogo kwa kutokuwa na mikataba ya uhakika mbele ya wafanyabiashara hao matajiri dhamira yake itashindwa kufikiwa mchana kweupe.

Wafanyabiashara hao licha kutoa mishahara duni tena isiyozingatia wakati,  wamekuwa wakikwepa kukusanya michango ya wafanyakazi wao na kuiwasilisha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama sheria inavyoelekeza.

Hali hiyo imewafanya wafanyakazi wengi kwenye sekta binafsi kuendelea kuwa "manamba" wasio kuwa na uhakika wa kesho itakuwaje kwa makato ya kipato chao kutowekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Aidha wafanyabiashara wamediliki kukiuka sheria kwa kutohakikisha usalama wa wafanyakazi sehemu za kazi, kutowaandikisha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, kutowaruhusu kujiunga na vyama vya wafanyakazi, hawatoi likizo za kawaida na hata za uzazi.

Kasoro nyingine za wazi ambazo zinakumbatiwa na wafanyabiashara hao ni kutolipa malipo ya ziada,wafanyakazi kutokuwa na siku ya kupumzika na kufanya kazi saa nyingi zaidi pasipo makubaliano ya aina yoyote.

Kwa mazingira hayo Dkt. Magufuli anapaswa kuleta mabadiliko chanya kwa kuwafanya wafanyabiashara hao kutimiza matakwa ya kisheria kwa wafanyakazi wao ili maisha yao yaendane na ukuaji wa pato la taifa.

Dkt. Magufuli amekuja na kauli mbiu ya "kutumbua majipu" ambayo yameota na kumea mahali ambapo hayakustahili kuwepo endapo uwajibikaji ungezingatiwa ipasavyo na serikali zilizotangulia.


No comments: