Na,
Murugwa Thomas, Tabora.
Mahakama
kuu kanda ya Tabora imeahirisha shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa
ubunge jimbo la Tabora mjini yaliyompa ubunge Emanuel Mwakasaka wa Chama
Cha Mapinduzi CCM hadi Jumatatu Februari
22 mwaka huu.
Shauri
hilo namba 3/2015 limeahirishwa kutokana na mawakili wa upande wa
walalamikaji Hashimu Mziray na Job Kiraria kushindwa kujibu
hoja za wajibu maombi zilizowasilishwa Mahakamani hapo na mawakili Juma Masanja
na Kamaliza Kayaga.
Kwa
upande wao wajibu maombi waliwasilisha pingamizi Mahakamani hapo wakitaka
shauri hilo liondolewe kwa vile walalamikaji hawakuwa na sababu za msingi
kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Akiahirisha
kesi hiyo jaji wa Mahakama kuu kanda ya Tabora Leilla Mgonya amewataka
mawakili wa walalamikaji wawe wamejibu hoja za pingamizi za wajibu maombi
kufikia jumatatu ijayo na kuonya kutoacha kufika mahakamani.
Amesema
kuwa mahakama kuu imejiwekea utaratibu kwamba kesi zote zinazohusu uchaguzi
zinapaswa kumalizika na kutolewa uhamuzi si zaidi ya mwezi Machi mwaka huu.
Katika
shauri hilo wanachama wanne wa Chama Cha Wananchi CUF Jumanne
Mtunda, Johari Kassanga, Shaban Mussa na Thomas Ayengo walifungua kesi Mahakama
kuu kupitia kwa wakili wao Mziray wakipinga uchaguzi uliofanyika na kumpa
ushindi Emanuel Mwakasaka wa CCM kwamba haukuwa huru na wa haki.
Awali
waleta maombi hao wanaopinga uhalali wa mbunge huyo wa CCM kushinda
uchaguzi huo waliomba Mahakama kupanga tarehe nyingine ya kuendelea
na shauri hilo kwa madai kwamba mawakili wao hawakufika kutokana na
majukumu mengine.
Hoja
ambazo hawajajibu ni pamoja na kuwasilisha ushahidi na vielelezo vya
kupinga matokeo hayo ikiwemo kwamba mlalamikiwa wa kwanza alitoa
rushwa ndipo akaweza kupigiwa kura wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
No comments:
Post a Comment