Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, February 24, 2016

ALCARDO ILAGILA:"NIMECHOKA KUCHAFULIWA KUHUSIKA KUIFILISI WETCU"




Na Hastin Liumba,Tabora

ALIYEKUWA mwenyekiti wa bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku kanda ya Magharibi (WETCU), Alcardo Ilagila amekanusha tuhuma kuwa yeye na bodi yake wamefilisi chama hicho hali ambayo ilipelekea bodi nzima kujiuzulu .

Akiongea na waandishi wa habari mwenyekiti huyo wa zamani amesema amekuwa akichafuliwa na bodi mpya ya sasa chini ya mwenyekiti wake Mkandala Gabriel Mkandala kuwa walishindwa kusimamia sheria na kanuni za ushirika hali ambayo iliisababishia hasara WETCU.

Ilagila amesema amekuwa akipigiwa simu na kuelezwa kwamba bodi mpya imekuwa ikiichafua bodi yake ambayo ililazimika kujiuzulu tarehe 23 Machi, 2013 kwa shinikizo la kupisha uchunguzi kuhusiana na tuhuma mbalimbali.

Amesema bodi mpya imeeneza uzushi kuwa yeye na bodi ya zamani aliyokuwa akioongoza waliacha benki kiasi cha Tsh mil. 7,000,000 tu jambo ambalo si kweli.

Mwenyekiti huyo wa bodi ya zamani ya WETCU amesema hadi kufikia tarehe 31 Machi ,2013  bodi yake iliacha benki Tsh. milioni 28,546,341.56.

Ilagila amefafanua kuwa katika akaunti ya benki ya CRDB kulikuwa na Tsh. mil. 23,323,559.88, NMB Tsh 829,230.96 na NBC Tsh mil.4,393,550.72.

Aidha amefafanua kuwa katika akaunti ya  benki za CRDB bodi yake iliacha dola za kimarekani  458,038.15, NMB dola 3,062.56 na NBC dola 78,806.

Kuhusu bidhaa ghalani amesema waliacha mbolea aina ya NPK 10:18:24 mifuko 15,366 katika wilaya za Urambo,Tabora na Sikonge, CAN27% N mifuko 60 katika wilaya ya Tabora mjini na UREA46% N mifuko 8,171 katika wilaya za Tabora,Urambo na Sikonge.

Ameongeza kuwa dawa ya kuua wadudu wa tumbaku iitwayo DECIS waliacha vidonge 50,965 katika wilaya za Tabora mjini na Sikonge ambapo dawa aina ya CONFIDOR ya kutibu makonyo waliacha Pakiti 4,268.

Ilagila amebainisha kuwa dawa ya maotea waliacha lita 2,552 katika wilaya za Tabora na Sikonge pamoja na magunia mapya ya kufungia tumbaku (NEW MISSIAN CLOTHES yenye urefu wa mita 1,165,188.

Ameweka wazi kuwa kasoro zilizopo sasa bodi yake haihusiki nazo kwani wanaamini walifanya vyema katika utendaji wao na kwamba bodi mpya imepita katika wilaya za Kaliua,Urambo,Sikonge na Uyui na kuongea na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika ikiipaka matope bodi ya zamani.
 
Ilagila amebainisha kuwa bodi mpya imekuwa ikiwaeleza viongozi hao wa vyama hivyo kuwa bodi ya zamani  ilifanya ubadhirifu na kwamba haikusimamia vyema sheria na kanuni za ushirika na hivyo kuisababishia hasara WETCU.

Mwenyekiti wa bodi mpya ya sasa Makandala Gabriel Mkandala alipohojiwa kuhusiana na malalamiko hayo amesema hana taarifa sahihi kama wajumbe wake wanaeneza hayo na hawezi kujibu chochote kwa kuwa amelazwa kwenye hospitali ya Nkinga wilayani Igunga.

“Sitazungumzia hayo kwa sasa hadi nitakapopata ushahidi lakini mimi
binafsi sihusiki  kueneza tuhuma hizo.”Amesema Mkandala.

No comments: