Ubunge jimbo la Tabora mjini utatolewa Ijumaa tarehe 26 Februari, 2016 baada ya mahakama kupokea majibu ya mapingamizi yaliyowasilishwa na
walalamikaji.
Hatua hiyo imefikiwa Jumatatu na jaji Leila Mgonya wa mahakama kuu kanda ya Tabora baada ya wakili wa wadai Job Keraria kujibu kwa majibishano badala ya maandishi mapingamizi yaliyowasilishwa na mawakili Kamaliza Kayaga na Juma Masanja wanaowawakilisha wadaiwa.
Awali jaji Mgonya alisema kuwa amekubali kupokea kwa majibishano
majibu ya mapingamizi hayo kutokana na kuzingatia misingi ya haki ili
maamuzi ya shauri hilo yaweze kutolewa mapema kama serikali
ilivyoelekeza.
Jaji mgonya alishangaa kuona mawakili wa waleta maombi kutochukulia
uzito madai yao kutokana na kitendo chao cha kuzembea kujibu hoja za
mapingamizi zilizowasilishwa na wajibu maombi kwa maandishi kama
walivyoelekezwa.
“Inaonekana walalamikaji walioleta shauri hili mahakamani
hawalichukulii katika uzito unaostahili” alisema jaji Mgonya.
Kufuatia hali hiyo wakili Kayaga alidai kwamba kutokana na waleta
maombi kushindwa kutekeleza amri ya mahakama iliyo tolewa tarehe 25
Januari mwaka huu basi inaonekana hawana majibu hivyo usikilizwaji uendelee .
Katika mapingamizi yao wakili Kayaga alidai mahakamani hapo kuwa
walalamikaji ambao ni wapiga kura hawana haki kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani kwa vile haki yao haikudhulumiwa.
Naye wakili Masanja anayemwakilisha mwanasheria mkuu wa serikali na
msimamizi wa uchaguzi alidai kwa vile walalamikaji walishiriki uchaguzi
na waliweza kupiga kura hawana madai yoyote kwa wateja wake.
Wakili Keraria alipinga hoja hizo na kusema kwamba walalamikaji wanayo haki kama raia zinazolindwa na sheria za nchi pamoja na kuzingatia matakwa ya katiba ambayo ndiyo sheria mama.
Wanachama wanne wa Chama Cha Wananchi (CUF) Jumanne Mtunda, Johari Kassanga, Shaban Mussa na Thomas Ayengo kupitia kwa wakili wao wanaiomba mahakama itengue matokeo ya uchaguzi huo uliompa ushindi Emanuel Mwakasaka wa CCM kwa madai haukuwa huru na wa haki.
Madai mengine ni kwamba mlalamikiwa wa kwanza alitoa rushwa ndipo
akaweza kupigiwa kura wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na kufanikiwa
kushinda.
No comments:
Post a Comment