Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, February 20, 2016

LIGI DARAJA LA TATU:WABISHI WA MJINI SABASABA FC WAWAFUNDISHA SOKA MAJIMAJI FC




Na Ramadhan Faraji, Tabora.

Kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora Jumamosi jioni Saba Saba FC “wabishi wa mjini” wametoa darasa la kusakata kabumbu baada ya kuichapa Maji Maji FC kwa magoli 4 kwa 1 katika mwendelezo wa ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa wa Tabora.

Licha ya mechi hiyo kuanza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, mvua iliyonyesha majira ya jioni ilitibua ladha ya utandazaji wa gozi la ng’ombe na badala yake ikawa butua butua kwa timu zote mbili.

Iliwachukua dakika 12 tu Maji Maji FC kuandika bao la kwanza kupitia kwa Steve aliyeunganisha mpira wa adhabu ndogo.

Kufuatia bao hilo Maji Maji FC iliendelea kulishambulia lango la wapinzani wao lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kuyatumia makosa ya yaliyofanywa na mabeki wa Saba Saba FC,Rajabu Konge na Nahodha Rajabu Ngonya kujipatia magoli.

Saba Saba FC “Wabishi wa mjini” walifufuka kimchezo na kunako dakika ya 38 mshambuliaji wake asiyekabika Sudi Sudi “Big” alifanyikiwa kuisawazishia timu yake baada ya kuyatumia vyema makosa yaliyofanywa na mabeki wa Maji Maji FC.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko zilikuwa zimafungana bao1 kwa 1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Saba Saba FC kucheza kwa kasi huku ikiwatumia walinzi wa kushoto na kulia kuongeza mashambulizi katika lango la Maji Maji FC.

Katika dakika ya 51 Saba Saba FC wakafanyikiwa kupata bao la pili lililofungwa na winga machachari Kamugisha Joseph, baada ya goli hilo ni dhahiri mpira ulionekana wa upande mmoja ambapo Saba Saba FC waliendelea kushambulia kwa kasi.

Mshambuliaji mwenye misuri wa Saba Saba FC Sudi Sudi “Big” aliachia shuti kali kunako dakika ya 72 lililomshinda mlinda mlango wa Maji Maji FC na kuandika bao la 3.

Kama haitoshi Wabishi wa Mjini wakaonyesha Ubishi wao wa kiume pale mchezaji wake Mashaka Juma alipomchambua golikipa wa Maji Maji FC na kuandika bao la 4 na la ushindi kwa Saba Saba FC.

Hadi mwamuzi wa kati anapuliza filimbi kuashiria kumalizika kwa mtanange huo Saba Saba FC 4 na Maji Maji FC 1 na hivyo kumfanya Kocha wa Saba Saba FC Mohamed Mdoma kutoka kitemi, kifua mbele na kumuacha mpinzani wake kocha wa Maji Maji FC John Protus akijiuliza ni wapi alipojichanganya.

Lgi hiyo ya daraja la tatu inaendelea tena Jumapili jioni katika uwanja huo wa Ally Hassan Mwinyi ambapo maafande wa JKT Msange watashuka dimbani kuvaana na watoto wa mjini Tabora FC.

No comments: