Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, February 20, 2016

EGPAF YABORESHA HUDUMA ZA AFYA HOSPITALI YA WILAYA YA IGUNGA




Na Allan Ntana, Igunga


HOSPITALI ya wilaya Igunga Mkoani Tabora imelipongeza Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (EGPAF) kwa mchango wake mkubwa uliowezesha hospitali hiyo kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa baba, mama na mtoto.

Pongezi hizo zimetolewa na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dr. Fidelis Mabula  alipokuwa akitoa taarifa ya hospitali kwa Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirika hilo Mercy Nyanda alipotembelea hospitali hiyo.

Dr Mabula amesema misaada mbalimbali inayotolewa na shirika hilo  imewezesha kupungua kwa maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI toka kwa mama mjamzito mwenye VVU kwenda kwa mtoto. 

Ametaja baadhi ya misaada iliyotolewa na EGPAF kuwa ni vifaa tiba, madawa, kuwezesha mafunzo mbalimbali kwa watoa huduma za afya ya uzazi (RCH) katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya hiyo na kutoa elimu ya namna ya kumkinga mtoto na maambukizi mapya toka kwa mama. 

Dr. Mabula amepongeza EGPAF kwa kuanzisha miradi mingi ya Afya ya uzazi kwa mama na mtoto katika wilaya hiyo ambayo pia inasaidia wakazi wa wilaya nyingine za jirani.

‘Shirika la EGPAF limetupa misaada mingi sana ambayo imetuwezesha kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa baba, mama na mtoto na kwa kiwango kikubwa  akinamama wajawazito na wanaonyonyesha wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuhudhuria kliniki.’ Amesema. 

Amesema mpaka sasa hospitali hiyo inajivunia uwepo wa vifaa vya kutosha vya huduma za RCH, PMTCT, CTC, CECAP, elimu ya kutosha kwa watoa huduma na upimaji maambuki ya VVU ikiwemo magari ya kwenda kutembelea vituo vya kutolea huduma hizo vijijini.

Dr Mabula amebainisha kuwa licha ya uwepo wa changamoto kadha wa kadha ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi na upungufu wa watoa huduma, timu yake  inafanya kazi ya kujituma, hivyo akahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kupima afya zao ikiwemo wanaume pamoja na wake zao. 

Naye Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi kwa baba, mama na mtoto wa wilaya hiyo Catherin Mushi ameeleza kuwa kuboreshwa kwa huduma za afya hospitalini hapo kumechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa huduma zote za wajawazito na dawa kwa wanaobainika kuwa na maambukizi ya VVU.

Aidha amesema kuwa kuboreshwa kwa huduma za RCH kumefanikiwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito ikiwemo kuzuia maambukizi mapya ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto sanjari na kuimarishwa kwa huduma za uzazi wa mpango.

No comments: