Timu ya taifa ya Mali imetinga fainali ya ubingwa
wa mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani CHAN 2016 nchini Rwanda
baada ya kuifunga Ivory Coast goli 1 kwa bila kwenye nusu fainali ya michuano
hiyo.
Mchezaji Yves Bissoouma wa Mali alifunga goli hilo
dakika ya 88 ya mchezo baada ya Hamidou Sinayoko kuugonga mpira kwa kichwa na
kumfikia mfungaji.
Katika kipindi cha kwanza mchezaji wa Ivory Coast,
Essis Aka alipiga shuti likagonga nguzo ya goli la Mali na baadaye penati
iliyopigwa na mchezaji wa Mali, Mamadou Coulibaly iliokolewa na golikipa wa
Ivory Coast, Ali Badra Sangare.
Kwa ushindi huo Mali itakutana na Congo DR kwenye
fainali itakayopigwa siku ya Jumapili Kigali nchini Rwanda.
Congo DR imefuzu kucheza fainali ya michuano ya
CHAN 2016 kufuatia ushindi wa penati 5 kwa 4 dhidi ya Guinea.
Congo DR na Guinea zilimaliza dakika 90 za kawaida
bila kufungana na katika muda wa nyongeza wa dakika 30 mchezaji wa Congo DR
Jonathan Bolingi alipachika goli kwa timu yake.
Lakini kabla ya dakika hizo za nyongeza kukamilika
Guinea kupitia kwa Sory Sankhon ilipata goli la kusawazisha, hadi mwisho wa
dakika 120 Congo DR 1 na Guinea 1.
Ndipo mikwaju ya penati ikaamuliwa na Congo DR
kuibuka na ushindi wa penati 5 kwa 4.
No comments:
Post a Comment