Na Paul Christian, Tabora.
Wakazi wa kata ya Mwinyi katika Manispaa ya Tabora
wamelilalamikia baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa hiyo kwa hatua yake ya
kupunguza kilometa nane kati ya kilometa kumi za barabara zilizotengewa bajeti
ya matengenezo katika maeneo korofi katani humo.
Mmoja wa wakazi wa kata hiyo Martha Mwijalubi
amesema kitendo hicho kimefanywa kwa makusudi ili kuwakomoa wakazi wa kata hiyo
kwa kumchagua diwani kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika
uchaguzi mkuu uliopita.
“Wingi wa madiwani wa chama tawala wameamua kuondoa
kilometa hizo za barabara na kuzigawa katika kata nyingine ambapo barabara zao
hazijaathiriwa sana na mvua zinazoendelea kunyesha.”Amebainisha mkazi huyo.
Alipohojiwa kuhusu suala hilo diwani wa kata hiyo Martin
Mussa Daniel kwa tiketi ya CHADEMA amekiri kuwa kikao cha baraza la madiwani kilichoketi
tarehe 23 na 24 Februari mwaka huu kwa kutumia wingi wa madiwani wa Chama Cha
Mapinduzi kilipitisha maazimio ya kuondoa kilometa nane za matengezo ya
barabara katika kata hiyo na kubakisha kilometa mbili tu.
“Kama mwakilishi wa kata hiyo nilijitahidi kujenga
hoja ya kutetea kilometa zote kumi zibaki kama ilivyopendekezwa kwa kuwa eneo
la Mwinyi lina wakazi wengi na barabara zake zimekuwa zikiathiriwa mara kwa
mara wakati wa msimu wa mvua.”Amesema diwani huyo.
Martin amebainisha kuwa ni dhahiri madiwani wa CCM
walikuwa wamejipanga kufanya hivyo kwa lengo la kudhoofisha uwakilishi wa
wananchi unaotokana na kumchagua mtu wa chama cha upinzani.
Ameongeza,“Hali hii itaathiri sana maendeleo ya
Manispaa ya Tabora kwa kutumia itikadi za kisiasa na wingi wa madiwani
wa CCM kupitisha maamuzi ya kukomoa wananchi wenye vyama na wasio na vyama kwa maslahi
duni ya kisiasa yanayolenga uchaguzi wa mwaka 2020.”
No comments:
Post a Comment