Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, March 7, 2016

SERIKALI YATOA TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO



TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 7 MACHI 2016

Ndugu Waandishi wa Habari,

Taarifa hii ni mwendelezo wa utaratibu ambao Wizara yangu imejiwekea kila wiki wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu hali ya kipindupindu nchini pamoja na kueleza juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hii.
Hadi kufikia tarehe 6 Machi 2016, jumla ya wagonjwa 17,369 wametolewa taarifa, na kati ya hao watu 269 wamepoteza maisha.

Takwimu za mwezi Februari zinaonyesha idadi ya wagonjwa imepungua kwa asilimia 10 ukilinganisha na idadi ya wangonjwa wa mwezi Januari, ambapo mwezi Januari kulikuwa na wagonjwa 2272 na Februari wagonjwa 1853.
Baadhi ya mikoa iliyokuwa inaongoza kuwa na wagonjwa wengi Januari 2016 kama Arusha na Simiyu, idadi ya wagonjwa  wapya imepungua. 

Kwa Mkoa wa Arusha, idadi ya wagonjwa imepungua kwa asilimia 47 kutoka wagonjwa 252 hadi 90 na kwa mkoa wa Simiyu idadi imepungua kwa asilimia 63 kutoka wagonjwa 265 hadi 59. 

Aidha mikoa ya Pwani, Tanga na Kagera ugonjwa huu umeweza kudhibitiwa kwani hakukuwa na mgonjwa mpya aliyetolewa taarifa ukilinganisha na Januari ambapo walikuwa wakitoa taarifa ya wagonjwa wapya kati ya 10-20. 

Mikoa ya  Dodoma, Mara na Mwanza imeendelea kuwa na idadi ya wagonjwa wapya wengi kwa mwezi wa Februari ukilinganisha  na mwezi Januari.

Aidha taarifa ya wiki iliyopita zinaonyesha kuwa kuanzia tarehe 28 Februari hadi 6 Machi 2016, idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa bado ni kubwa yaani 544 ambayo ni ongezeko la asilimia 7 na kati yao watu 11 walipoteza maisha. 

Aidha Mikoa iliyokuwa ikiripoti ugojwa wa kipindupindu imepungua kutoka Mikoa 12 hadi 10, japo takwimu bado zinaonyesha bado idadi ya wagonjwa iko juu. 

Mkoa wa Morogoro umeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ambayo ni 114, ukifuatiwa na mkoa wa Mara wenye wagonjwa 107 na mkoa wa Dodoma wenye wagonjwa 107. 

Mkoa wa Iringa ambao ulikuwa ukiongoza kuwa na idadi kubwa ya wagojwa kwa sasa hauna mgojwa aliyeripotiwa.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Vikosi kazi vya wataalamu kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanaoendelea kuzuru maeneo mbalimbali wameendelea kutoa mwongozo wa kisera na kitaalam katika kudhibiti kipindupindu na vile vile kuibua changamoto mbali mbali na kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili kuzuia ueneaji wa vimelea vya ugonjwa huu na kisha kuutokomeza kabisa.

Moja ya changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza ni pale ambapo baadhi ya wataalam wa afya wa ngazi mbalimbali kutozingatia taratibu za utoaji taarifa wakati wa magonjwa ya mlipuko kama zilivyoanishwa kwenye miongozo mbalimbali ya Wizara.

Ndugu waandishi wa habari,

Wizara imebaini kuwa ushirikishwaji wa viongozi wa ngazi ya chini ya kijiji, kama wenyeviti wa serikali za mitaa, afisa mtendaji wa kijiji na wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika mapambano dhidi ya kipindupindu ni jambo muhimu sana na limeleta mafaniko makubwa ya kupungua kwa ugonjwa.
Aidha Wizara inatoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu

Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:

·         Utoaji na upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara bila kuingiliwa na viongozi wa kisiasa au kiserikali

·        Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mjini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.
·       
 Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia Mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote.
       
·        Kuhakikisha upatikanaji wa ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini na watu mashuhuri wasaidie kuhamasisha jamii zao kuhusu ugonjwa huu.
·       
Kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa
·        Kuwahi kupata matibabu mapema katika vituo vya kutolea huduma
       
·        Kuhakikisha upatikanaji na matumizi sahihi ya ORS katika maeneo mbali mbali nchini ili kupunguza athari za ugonjwa


Hitimisho

Wizara inaendelea kuwashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada za kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Aidha tunawashukuru na kuwapongeza watumishi wa afya katika ngazi mbali mbali kwa juhudi zao katika kupambana na ugonjwa huu.

Hata hivyo Wizara inapenda kutoa wito kwa mikoa hiyo na mikoa mingine ambayo ugonjwa unaelekea kudhibitiwa kutobweteka na kuendelea na jitihada za udhibiti, kwani uwezekano wa ugonjwa kuibuka tena bado upo.

Pia tunawapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kuisaidia Serikali kuielimisha jamii jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.

Asanteni sana

No comments: