REHEMA KABATA |
Na Paul Christian,Tabora.
CHAMA Cha Wananchi CUF wilaya ya Tabora kimeitaka
serikali ya mkoa wa Tabora kuingilia kati maazimio ya baraza la Madiwani wa
halmashauri ya manispaa ya Tabora kuahamisha mradi wa ujenzi kutoka zahanati ya
Town Clinic kata ya Chemchem na kuupeleka kata ya Ifucha.
Akizungumza na Tabora Watch Diwani wa kata ya
Chemchem katika manispaa hiyo kwa tiketi ya CUF Rehema Kabata amesema baraza
hilo la madiwani limetumia wingi wa madiwani wa chama tawala kupitisha maazimio
yanayoathiri kata zinazongozwa na vyama vya upinzani.
Amesema Mradi huo wa ujenzi wa wodi ya wazazi
pamoja na chumba cha kujifungulia akinamama wajawazito wenye thamani ya
shilingi milioni 100,004,000 ulikuwa kwenye mkakati wa utekelezaji tangu mwaka wa
fedha wa 2014/2015 hadi mwaka wa fedha 2016/2017 ulipopata fedha hizo.
Diwani Kabata amefafanua kuwa kikao cha madiwani
wa halmashauri hiyo kilichoketi Februari
23 na 24 mwaka huu kupitia wingi wa madiwani wa Chama Cha Mapinduzi kiliazimia
mradi huo kuhamishwa kutoka kata ya Chemchem na kupelekwa kata ya Ifucha kwa
hoja dhaifu ya kusaidia watu wa kata za pembezoni.
Amebainisha kuwa mradi huo uliolengwa kutekelezwa
kwenye zahanati ya Town Clinic ulilenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya
afya ya mama na mtoto kwa wakazi wa kata sita ambazo ni Chemchem, Mwinyi, Kanyenye,Gongoni,Mbugani
na Tambuka Reli katika Manispaa hiyo.
Diwani huyo ameeleza kuwa zahanati ya Town Clinic
ni kongwe na iko kwenye kata yenye wakazi 14,453 wenye uwezo wa kufanya kazi ambao
kimsingi wangenufaika na mradi huo ambao umehamishiwa kwenye kata ya Ifucha
yenye wakazi 3,307 wenye uwezo wa kufanya kazi.
Kabata akifafanua zaidi amesema, “katika kipindi
cha tarehe 18 Januari na tarehe 28 Februari mwaka huu katika zahanati hiyo
akinamama 48 wamejifungulia hapo ukilinganisha na zahanati ya Ifucha katika
kipindi hicho ilihudumia akinamama watatu kujifungua.”
Amefafanua kuwa katika kata ya Chemchem miongoni
mwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wanawake ni 5,975 wakati katika kata ya
Ifucha miongoni mwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wanawake ni 1,607.
Kabata amesema, “Zahanati ya Town Clinic kupitia
mfuko wa bima ya Afya imeteuliwa kuwa kituo cha tiba kwa kadi (TIKA) na hivyo
kuifanya kuhudumia akinamama wajawazito 32,988.”
Ameongeza, “katika mazingira hayo ni dhahiri kuwa
wanasiasa wametumia nafasi zao vibaya kuwaumiza wananchi kwa maslahi ya kisiasa
kuangalia uchaguzi wa mwaka 2020.”
Aidha katibu wa Chama Cha Wananchi CUF wilaya ya
Tabora Kapasha H. Kapasha ameandika barua ya terehe 1 Machi mwaka huu kwenda
kwa mkuu wa mkoa wa Tabora kumtaka kuingilia kati maazimio hayo ya baraza la
madiwani.
No comments:
Post a Comment