Maofisa watendaji wawili wa kata na
kijiji katika halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wamefikishwa
mahakamani wakikabiliwa na mashitaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa ya
shilingi 700,000/=.
Akiwasomea mashitaka mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Tabora Emanuel Ngigwana, wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Edson Mapalala alisema watuhumiwa hao Alfred Mashaka afisa mtendaji wa kata ya Kiloleli na Thomas Dickson mtendaji wa kijiji cha Kanyamsenga walitenda makosa hayo Januari 4 mwaka huu.
Wakili huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa
katika shitaka la kwanza watuhumiwa hao waliomba kiasi hicho cha
fedha toka kwa Masuluzi Samweli ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kosa la
kumpiga Mabula Sinyaka.
Mapalala aliongeza kuwa katika
shitaka la pili watuhumiwa wakiwa
ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge kwa pamoja
walipokea shilingi 700,000/- toka kwa Masuluzi kama kishawishi na kushindwa
kumchukulia hatua za kisheria.
Upande wa mashitaka kupitia kwa
wakili Mapalala uliiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo
umekamilika na kuomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza usikilizwaji
wa awali.
Watuhumiwa wote walikana mashitaka
dhidi yao na wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya
dhamana kwa kutokuwa na watu wenye sifa hadi tarehe 29 Machi 2016 shauri hilo
litakapoanza usikilizwaji wa awali.
No comments:
Post a Comment