AGGREY MWANRI |
Na Paul Christian,Tabora.
Wamiliki wa asili wa shamba la miti lililotumika
kama shamba darasa katika miaka ya 1970 kata ya Malolo katika Manispaa ya
Tabora wamemuomba mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kuingilia kati mgogoro
kati yao na halmashauri ya Manispaa ya Tabora ambayo imetamka kulichukua shamba
hilo.
Akizungumza kwa niaba ya familia tatu zinazohusika
na mgogoro huo Bi Rukia Manyama amesema mnamo tarehe 8 mwezi wa pili mwaka huu
alimwandikia barua mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa hiyo akiomba
kupimiwa eneo hilo lililotumiwa kama shamba darasa wakati wa kampeni ya
upandaji miti katika miaka hiyo ya 1970.
Amesema baada ya kuandika barua hiyo mkurugenzi
huyo alimjibu kwa barua ya tarehe 23 mwezi wa pili mwaka huu na kusainiwa kwa
niaba yake na Suzana Pinini Mizengo ambapo pasipo kufafanua zaidi alieleza kuwa
eneo hilo lilitwaliwa na serikali katika miaka ya 1970.
Akitoa ushahidi wake aliyekuwa afisa misitu wa
serikali wakati huo Hussein Mchemba mnamo tarehe mosi mwezi wa sita, 2015
alimwandikia barua mkurugenzi huyo akimweleza kuwa eneo hilo lililotumika kama
shamba darasa liliazimwa na serikali kwa lengo la kufundishia wananchi namna ya
upandaji miti na sio kweli kwamba lilitwaliwa na serikali.
Katika barua hiyo ameongeza kuwa serikali
ilikubaliana na familia hizo tatu kuwa endapo miti hiyo itakua na kuvunwa ardhi
hiyo itarejea kwa wamiliki wa asili ambao ni familia ya Rukia Kanyama, Rashid Kambi na Cheko Masai.
Aidha katika barua hiyo Mchemba alimkumbusha Mkurugenzi huyo kuwa ni utaratibu upi uliotumika kuitwaa ardhi hiyo wakati sheria za nchi zinamaelekezo na kwa nini usitolewe ushahidi unaothibitisha kuwa serikali ililitwaa eneo hilo kisheria .
No comments:
Post a Comment