Timu ya Chad iliyokuwa icheze na timu ya taifa ya Tanzania “Taifa
“Stars” kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumatatu Jioni,haitofika Tanzania baada ya
kujitoa katika kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika
AFCON 2017 zitakazochezwa nchini Gabon.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa Jumapili na katibu mkuu wa
chama cha Soka nchini humo FTFA Moctar Mahamoud kwenda Shirikisho la Soka Barani
Afrika CAF imeeleza kuwa Chad imeshindwa kufika Dar es Salaam kucheza mechi ya
marudiano kwa madai kuwa haina fedha za
kuwawezesha kuendelea na mechi za kundi G.
Taifa hilo la Chad limejitoa baada ya kucheza mechi tatu za
mzunguko wa kwanza, huku ikifungwa na timu zote, ambapo ikicheza ugenini ilifungwa
na Nigeria bao 2 kwa 1,ikiwa kwenye ardhi ya nyumbani ikafungwa magoli 5 kwa 1
na Misri, na tarehe 23 mwezi huu ikashindwa kutamba mbele ya Tanzania baada ya
kukubali kichapo cha bao 1 kwa bila ikiwa nyumbani.
Kwa hatua hiyo ya Chad,kundi G limebaki na timu tatu za Tanzania,
Misri na Nigeria.
Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Shirikisho la Soka Barani
Afrika CAF kujitoa kwa Chad kumesababisha kufutwa kwa matokeo yote ya timu
hiyo, na hivyo kulifanya kundi G kuongozwa na Misri ikiwa na pointi 4 badala ya
7, Nigeria ya pili ikiwa na pointi 2 badala ya 5 na Tanzania inashika mkia
ikiwa na pointi moja badala ya 4.
Aidha CAF imeitoza Chad faini ya dola za kimarekani 20,000
pamoja na kupigwa marufuku kushiriki hatua za kufuzu fainali za AFCON mwaka 2019.
Hata hivyo Misri ikiwa nyumbani katika mji wa Alexandria
wataikaribisha Nigeria katika mechi ya marudiano itakayochezwa Jumanne ya
tarehe 29 mwezi huu baada ya mechi ya kwanza kuchezwa katika mji wa Kaduna na
kutoka sare ya kufungana bao 1 kwa 1.
Kujitoa kwa Chad kumeyabakiza mataifa 50 ya Afrika yakiwania
nafasi 15 za kufuzu fainali hizo za AFCON
ambapo zitaungana na mwenyeji Gabon na kukamilisha idadi ya timu 16.
Timu zitakazoongoza katika makundi yote 13 zitafuzu moja kwa
moja kwenye fainali hizo na washindi wa pili wawili bora kutoka miongoni mwa
makundi 12 ukiondoa kundi la kwanza lenye timu mwenyeji Gabon zitafuzu pia.
Hata hivyo Kamati ya Utendaji ya Shirikisho La Soka Barani
Afrika CAF Mnamo tarehe 15 Januari,2015 ilipitisha uamuzi kwamba timu zikibaki
tatu kwenye kundi ni timu moja tu ambayo itaoongoza kundi hilo ndio itafuzu
fainali za AFCON.
Timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” itashuka kwenye uwanja
wa taifa jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi ya tarehe 4 Juni, 2016 kucheza
na Misri.
No comments:
Post a Comment