Na Paul Christian, Tabora.
Mpango
wa kunusuru kaya masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF
awamu ya tatu unakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na takwimu sahihi ya idadi
ya watoto wanaostahili kupata fedha za ruzuku ya masharti.
Mratibu
wa TASAF mkoa wa Tabora Ngoko Buka amebainisha hayo wakati wa ziara ya
kutembelea zoezi la kutoa fedha za ruzuku ya msingi na ya masharti kwa kaya
masikini katika kata za Usoke,Ugalla na Uyumbu wilayani Urambo.
Amesema
takwimu sahihi ya wanufaika wa ruzuku ya masharti inayotolewa kwa watoto
wanaosoma shule za msingi na sekondari pamoja na wale wenye umri chini ya miaka
mitano wanaohudhuria kliniki kutoka kaya masikini haijulikani kikamilifu
kutokana na sababu mbalimbali.
Ngoko
amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na wakati wa zoezi la kuzitambua kaya
masikini baadhi ya watoto waliandikishwa majina tofauti na yale wanayoyatumia
shuleni hivyo kutoonekana kwenye madaftari ya mahudhurio katika shule husika.
Amesema
sababu ya pili ni baadhi ya watoto kutoka kaya masikini kusoma kwenye shule za
vijiji jirani tofauti na vijiji ambavyo kaya husika zinaishi hali ambayo
imewafanya watoto hao kutokuwepo kwenye madaftari ya mahudhurio katika shule za
vijiji wanavyoishi.
Mratibu
huyo wa TASAF mkoa wa Tabora amesema kasoro hizo zimewafanya baadhi ya watoto
kuondolewa kwenye orodha ya watoto wanaostahili kupata ruzuku ya masharti kwa
madai ya kukiuka masharti kwa kutohudhuria masomo jambo ambalo sio sahihi.
Aidha
Ngoko amebainisha kuwa katika shule za msingi na sekondari walimu wanapojaza
fomu maalum za TASAF kuonyesha mwenendo wa mahudhurio hawana orodha ya
wanafunzi wanaonufaika kutoka kaya masikini ambayo inaainisha idadi yao na
madarasa wanayosoma.
Amesema
ukosefu wa orodha ya wanafunzi kutoka kaya masikini inasababisha walimu
kukabiliwa na ugumu wa kufanya rejea wakati wa ufuatiliaji wa mahudhurio ya
wanafunzi hao hali ambayo imefanya kuwe na ugumu wa kupata takwimu za moja kwa
moja katika shule hizo.
Mratibu
huyo ameainisha kasoro nyingine iliyojitokeza ni walimu kulalamikia kutokuwa
sehemu ya mpango wa kunusuru kaya masikini na badala yake wamekuwa wakitumika
kama wajaza fomu za TASAF hali inayochangia kutowajibika ipasavyo.
Katika
kukabiliana na changamoto hizo, Ngoko amewaagiza watendaji wa vijiji, walimu
pamoja na wazazi au walezi wenye wanafunzi kutoka kaya masikini kukaa kwa
pamoja na kuondoa kasoro zilizopo kwa kubaini majina sahihi ya wanafunzi na
shule wanazosoma ili wanufaike na mpango kama ilivyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment