Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, March 21, 2016

DC SIKONGE AONYA MAKAMPUNI YANAYOCHELEWESHA MALIPO YA WAKULIMA WA TUMBAKU



 
TUMBAKU
Na Allan Ntana, Sikonge

MAKAMPUNI yanayojishughulisha na ununuzi wa zao la tumbaku toka kwa wakulima wilayani Sikonge Mkoani Tabora yameonywa vikali na kutakiwa kuacha mara moja tabia iliyozoeleka ya kuchelewesha malipo ya wakulima hao.

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Hanifa Selengu katika
kikao maalumu cha ‘Wadau wa Tumbaku’ kilichofanyika Jumamosi katika ukumbiwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) wilayani humo.

Amesema tabia ya kuchelewesha malipo ya wakulima wa tumbaku
inayofanywa na makampuni yanayonunua zao hilo imekuwa kero kubwa kwa wakulima hao na kwa kiasi kikubwa imechangia umaskini wao kwani
hawapati fedha yao kwa wakati muafaka na hata wakiipata inakuwa na
makato mengi.

‘Mkulima anapovuna tumbaku yake anauhakika kuwa atauza na atapata
fedha, lakini inapotokea analipwa hela kidogo na nyingine kutojulikana
ni lini italipwa linawakwaza sana, ukweli siko tayari kuendelea kulea
makampuni ya namna hiyo, nitawatimua wilayani kwangu’, ameonya.

Ametaja baadhi ya makampuni yanayonunua tumbaku wilayani humo kuwa ni TLTC, Alliance One na JTI na kutoa onyo kali kwa kampuni yoyote ambayo
haijamaliza kulipa hela za wakulima hao.

‘Msimu mpya wa masoko kwa mwaka huu unaanza mwezi wanne, ikifika
wakati huo kabla hamjawalipa malipo yao yote muondoke katika wilaya
yangu na sitaruhusu kampuni yoyote kujihusisha na ununuzi wa tumbaku
tena, huu ni wizi,’ amesisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Aidha amebainisha kuwa serikali imefuta rasmi uwepo wa vyama vya
ununuzi wa tumbaku vya wakulima binafsi (IF) ili kuepusha migongano ya
wakulima hao na kuongeza kuwa wote wanapaswa kujisajili katika vyama
vya msingi vilivyopo, labda itakapoamriwa vinginevyo.

Mwakilishi wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku (WETCU) amewaelezawadau hao kuwa kwa kuwa hizi ni zama mpya za uongozi wa UNION hawatakuwa tayari kuendelea kulea vitendo vya ujanja ujanja,wizi na ulaghai wa makampuni hayo bali watasimamia haki ya kila mkulima.

Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa kuanzia sasa watakuwa wanaishirikisha serikali katika upangaji bei za tumbaku ili kuyabana makampuni yasiyofuata utaratibu wa bei elekezi za ununuzi wa tumbaku.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Peter Nzalalila amesema
baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku
wamekuwa mzigo kwa wanachama wao,wanafanya maamuzi mengi pekee yao kwa maslahi binafsi.

Hivyo akaonya vikali tabia za viongozi hao kwani zinachangia kuwanyonya wakulima ikiwemo kuwacheleweshea malipo yao na kuwaingiza katika madeni yasiyoeleweka na wakati mwingine huchukua mikopo benki
pasipo kuwashirikisha.

No comments: