Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Tuesday, March 15, 2016

DC HANIFA SELENGU, “TUMETENGA MILIONI 360 ZA KUTENGENEZA MADAWATI”



PICHA KUTOKA MAKTABA
Na Allan Ntana, Sikonge.
 
HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imeanza zoezi la
kutengeneza madawati  5,000 ili kufanikisha azma ya serikali ya
awamu ya 5, kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu kila mwanafunzi awe anakaa kwenye dawati. 

Akizungumza ofisini kwake Jumatatu, mkuu wa wilaya hiyo Hanifa Selengu amesema wilaya yake tayari imetenga kiasi cha shilingi milioni 360 kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo.

Amesema zoezi la kutengeneza madawati hayo limeanza na linatarajiwa
kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu ambapo mafundi walioingia
mkataba na halmashauri hiyo watayakabidhi kwa uongozi wa wilaya ya
hiyo.

“Zoezi la kutengeneza madawati 5000 tayari limeanza kwa kasi,
nimemweleza mkandarasi anayefanya kazi hiyo ahakikishe ifikapo mwezi
Mei mwaka huu awe amekabidhi madawati yote yakiwa yamekamilika na si vinginevyo.” ameongeza.

Mkuu huyo wa wilaya amefafanua kuwa madawati yanayotengenezwa ni ya bomba za chuma na juu yake wataweka topu za mbao na kwamba kila dawati litatumiwa na wanafunzi wawili.

“Wilaya yangu imekuwa ya kwanza kimkoa kwa kufaulisha wanafunzi wa
kuingia sekondari kwa asilimia 75, nina uhakika kukamilika kwa
madawati hayo na kila mtoto akakaa kwenye dawati  kutaongeza
ufaulu wao kwa kiwango kikubwa  zaidi.”Amebainisha Selengu

Akizungumzia zoezi hilo akiwa kwenye eneo la karakana yanakotengenezwa
madawati hayo, Afisa Manunuzi wa wilaya hiyo Felix Mkilya amesema
mpaka sasa asilimia 50 ya vifaa vyote vinavyotakiwa kwa kazi hiyo
zikiwemo mbao na mabomba ya chuma vimeshafika.

Amesema kuwa hadi sasa mbao (aina ya mtundu) zipo za kutosha na
mabomba ya chuma 6000 (square pipe) tayari yameshafika kwenye karakana na kazi imeshaanza na kila dawati litagharimu kiasi cha sh 75,000/- bila VAT.

Fundi Mkuu anayesimamia kazi hiyo, Eliaza Masano Musiba amesema zoezi
hilo linaendelea vizuri na ana uhakika kazi hiyo itamalizika ndani ya
muda uliopangwa huku akibainisha kuwa ameagiza mafundi wengine kutoka Manispaa ya Tabora ili kuongeza nguvu zaidi.

Aidha amebainisha kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme ingawa anafanya jitihada ya kupata jenereta la dharura.

No comments: