Na
Thomas Murugwa, Tabora.
Taasisi
ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Tabora imemkamata na
kumfikisha mahakamani afisa mtendaji wa kijiji Utimle wilayani Sikonge kwa kosa
la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 50,000/-.
Akisoma
mashitaka dhidi ya mshitakiwa huyo Batholomeo Athanas Sonda mbele ya hakimu wa
mahakama ya mkoa wa Tabora Jackton Rushwela wakili wa TAKUKURU Edson Mapalala
alisema mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo mjini Sikonge kati ya tarehe mosi na
pili Machi mwaka huu.
Wakili
huyo wa TAKUKURU alidai mahakamani hapo
kuwa mtendaji huyo wa kijiji mnamo tarehe 1 Machi 2016 akiwa kwenye eneo
la stendi ya mabasi ya Sikonge aliomba shilingi laki nne kutoka kwa Hussein
Hamis Swalehe ili amruhusu aendelee kuvuna mazao ya misitu.
Ilidaiwa
katika shitaka la pili kuwa mtuhumiwa alipokea shilingi elfu 50,000/= toka kwa
Swalehe ikiwa kama kishawishi ili amruhusu aendelee kuvuna mazao ya misitu bila
kuwa na kibali toka kwa mkurugenzi wa maliasili.
Mtendaji
huyo amekana makosa yote mawili na kesi hiyo impangwa kutajwa tarehe 5
Aprili 2016 ili ipangiwe tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu
Rushwela alikubali mtuhumiwa apewe dhamana ya watu wawili kwa ahadi ya shilingi
milioni tano na kutoa masharti kwamba mmoja wa wadhamini awe ni mkazi wa
manispaa ya Tabora ili iwe rahisi kumpata mtuhumiwa pindi anapohitajika.
Masharti
hayo yamewekwa na mahakama kwa kile kilichodaiwa kuwa watuhumiwa wengi
wanapodhaminiwa na wakazi wa nje ya manispaa ya Tabora wamekuwa
wanashindwa kufika mahakamani na hivyo inakuwa ni vigumu kuwapata ili wajibu
mashitaka yao.
Hii
ni mara ya pili kwa watendaji wa vijiji vya wilaya ya Sikonge kufikishwa
mahakamani mkoani hapa wakikabiliwa na mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa
katika kipindi kisichozidi wiki mbili.
Machi
23 mwaka huu TAKUKURU iliwafikisha mahakamani Alfred Mashaka afisa
mtendaji wa kata ya Kiloleli na Thomas Dickson afisa mtendaji wa kijiji cha
Kanyamsenga kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki saba.
No comments:
Post a Comment