Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
limeagiza Chama Cha Soka Mkoa wa Katavi (KRFA) kufanya uchunguzi wa matokeo ya
timu ya Stand FC kuibuka na ushindi wa magoli 16 kwa 0 dhidi ya Kamazima wakati
wa mechi ya kuamua bingwa wa mkoa wa Katavi.
Mechi hiyo ilichezwa Jumamosi ilikuwa ya
kuhitimisha kumpata bingwa wa mkoa huo atakayewakilisha kwenye ligi ya mabingwa
mkoa ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kabla ya mchezo huo uliotoa matokeo ya
kushangaza, timu ya Nyundo FC ilikuwa inaongoza kwa kuwa na pointi 21 na magoli
24 ya kufunga ambapo Stand FC ilikuwa ikihitaji kufunga magoli 13 kwa 0 ili
iweze kuwa mabingwa wa mkoa huo
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
TFF imeeleza kuwa kutokana na Stand FC kushinda kwa mabao 16, inaonyesha kuna
dalili za kupanga matokeo, hivyo KRFA haitaruhusiwa kutangaza bingwa wa mkoa wa
Katavi hadi uchunguzi utakapokamilika na TFF kujiridhisha na uchunguzi huo.
Hivi karibuni TFF ilizuia kuitangaza
timu iliyopanda daraja kutoka Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza kutokana na
madai ya kuwepo kwa vitendo kama hivyo ambapo katika mechi za mwisho, Geita
Gold Sport iliifunga JKT Kanembwa magoli 8-0, huku Polisi Tabora ikiifunga JKT
Oljoro mabao 7-0.
No comments:
Post a Comment