Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Tuesday, March 1, 2016

KIKWETE APONGEZWA KUTEULIWA KUWA BALOZI WA HESHIMA WA CHANJO DUNIANI



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA



TAARIFA KWA UMMA KUFUATIA KUTEULIWA KWA MHESHIMIWA RAIS MSTAAFU DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KUWA BALOZI WA HESHIMA WA CHANJO DUNIANI KUPITIA SHIRIKA LA GAVI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kwa furaha uteuzi uliofanywa na Shirika la Global Alliance for Vaccines and Immunizations (GAVI) kwa  kumteua Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais  Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Balozi wa Heshima wa Chanjo Duniani. Kwa niaba ya Serikali, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa niaba yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huu.

Ndugu wananchi, 

Kama mlivyosikia kwenye vyombo vya habari  Rais wetu mstaafu wa awamu ya nne (4) Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuwa BALOZI WA HESHIMA WA CHANJO DUNIANI kupitia shirikia laGlobal  Alliance for Vaccines  and  Immunizations (GAVI) mnamo tarehe 31Januari,2016 nchini Ethiopia.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kuchukua fursa hiikuungana na shirika la GAVI pamoja na wananchi wote wa Tanzaniakumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huo. Kuteuliwa  kwake kuwa Balozi wa heshima kwenye masuala ya chanjo, kuna maana ya kuwa,atakuwa mhamasishaji wa  wakuu wote wa nchi  za Afrika na dunia kwa ujumla kuhakikisha  wanaweka kipaumbele katika  upatikanaji wa huduma za afya hususan masuala ya chanjo.

Katika muda wote wa uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa kipaumbele  katika  masuala ya afya ya uzazi  na  mtoto  likiwemo suala la chanjo   na  kuhakikisha wanawake na watoto  wanapata huduma ipasavyo.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Watanzania wote tumefarijika sana kwa uteuzi huo, kwani pamoja na juhudi hizo, amekuwa  ni Mwenyekiti mwenza wa Jopo la watu mashuhuri la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  juu ya uboreshaji wa malengo ya  Maendeleo  endelevu.(Sustainable Development Goals)

Aidha,Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alishiriki katika mkutano mkubwa wa GAVI uliofanyika mnamo tarehe 26 hadi 27Januari  2015 nchini Ujerumani na kueleza dhamira yake na ya nchi kwa ujumla katika kushiriki kikamilifu kupunguza kiwango kikubwa cha maradhi na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,Tanzania iliweza kuongeza kiwango cha  utoaji wa huduma za chanjo hadi  kufikia  wastani wa zaidi ya asilimia 95 ikiwa ni zaidi ya lengo la Kimataifa la  asilimia  90.Tunaami kuwa mafanikio haya yamechangia Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kupewa heshima hiyo.

Historia inaonyesha kuwa kwenye miaka ya sabini watoto wengi walipoteza maisha yao kutokana na magonjwa yanayozuilika  kwa chanjo.Wengi wetu ni mashahidi wa milipuko na vifo vilivyotokana na ugonjwa wa surua kipindi hicho. Wodi nyingi katika Hospitali zetu zilitengwa na zilijaa watoto waliougua surua na ugonjwa wa pepo punda.  Aidha, watoto wengi  walibakia na ulemavu wa viungo, ulemavu wa kutoona, ulemavu wa kutosikia,  na mtindio wa ubongo kutokana na athari za magonjwa ya polio na  surua.

Juhudi za Serikali katika kukabiliana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo zimeleta mafanikio makubwa. Kwa mfano, magonjwa ya ndui na pepopunda kwa watoto wachanga yametoweka,pia tumeshuhudia wodi za surua zikifungwa, na vifo vitokanavyo na surua kupungua kwa kiasi kikubwa.Aidha Tanzania imekwisha thibitishwa kuwa ni miongoni mwa nchi zilizotokomeza ugonjwa wa Polio duniani. Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za Serikali  kuwekeza katika chanjo.

Imethibitika kuwa chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza magonjwa  na kupunguza vifo vya watoto, hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia zetu na Taifa kwa ujumla lingetumia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Rejea za kitaaluma zimethibitisha kuwa chanjo huzuia takribani vifo Milioni 2 hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika  kwa chanjo duniani. Nchini Tanzania,  mwaka 2004, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 112 kati ya vizazi hai 1,000 na viliendelea kupungua hadi vifo 81 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2010.

Mojawapo ya mikakati ya Mheshimiwa  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika kipindi chake cha uongozi ilikuwa ni kufikia malengo ya maendeleo ya Milenia. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa (UN Inter Agency Report for child mortality estimates), Tanzania ilifanikiwa kufikia lengo la Millenia namba 4 la kupunguza vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka 5 kutoka vifo 81 hadi vifo 54 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2013.

Tunafahamu kuwa Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ana kazi kubwa mbele yake ya kuhakikisha nchi zote za Afrika na Dunia kwa ujumla zinafikia kiwango cha wastani wa asilimia 90 wa chanjo kwani, hadi sasa,  bado kuna nchi ambazo bado zina kiwango cha wastani wa asilimia 50.

Ni faraja yetu kubwa  kuwa Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ataendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha  upatikanaji wa huduma za chanjo barani  Afrika na dunia kwa ujumla na hivyo kuokoa maisha ya watoto. 
 
Tunamtakia mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu hayo makubwa kidunia,na kumuahidi ushirikiano wetu.

Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
1.3.2016

No comments: