Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, March 26, 2016

MWENYEKITI WA KIJIJI AUAWA NA KUCHOMWA MOTO





Na, Thomas Murugwa , Sikonge.

Mwenyekiti wa halmashauri ya kijiji cha Makibo wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Petro Ntakulo ameuawa kwa kukatwa mapanga na mwili wake kuchomwa moto na watu wasiojulikana na kisha kutoweka.

Taarifa iliyotolewa na kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Hamis Issa amesema tukio hili limetokea  Machi 21 mwaka huu majira ya saa 4:30 usiku katika kijiji cha Makibo kilichopo Kata ya Nyauha Wilayani Sikonge.

Akielezea tukio hilo amesema ilitokea sintofahamu iliyosababisha watu kukusanyika kujua nini kimetokea ndipo watu hao wasiojulikana walimvamia mwenyekiti huyo kisha kumkatakata mapanga na kuuteketeza mwili wake kwa moto.

Kamanda Issa amefafanua kuwa hadi sasa chanzo cha mauaji hayo hakijulikani na kwamba maafisa wa jeshi hilo  kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kufanya uchunguzi.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya mashuhuda ambao hawakutaka majina yao yafahamike wamesema mauaji hayo yalitokea baada ya kupigwa mwano kuashiria jambo la hatari, wanakijiji walikusanyika pamoja na mwenyekiti huyo ndipo watu hao wasiofahamika wakatekeleza
mauji hayo.

Aidha wameeleza kuwa watu hao pia waliichoma moto nyumba na mali zilizokuwemo kwenye nyumba ya mwenyekiti huyo huku wakitamka kuwa hawataki kuwaona viongozi wa serikali pamoja na wazee.

Katika hatua nyingine mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge
Peter Nzalalila amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi
na badala yake wafuate sheria kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za
nchi.

No comments: