Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, April 27, 2016

UKATAJI MITI UNAHATARISHA HALI YA HEWA YA MKOA WA TABORA



Na Hastin Liumba,Tabora 

Diwani wa kata ya Gongoni manispaa ya Tabora Kessy Sharrif Abdulrahman amewaasa wakazi wa kata hiyo na maeneo mengine kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda miti.

Amesema suala la kupanda miti linapaswa kuwa ajenda ya kudumu kwa wakazi wa mkoa wa Tabora ambao kwa sasa umeanza kuathiriwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti kwa matumizi mbalimbali.

Abdulrahman amebainisha kuwa maeneo ya mkoa wa Tabora kwa sasa yameanza kukabiliwa na uhaba wa mvua na ongezeko la joto tofauti na miaka iliyopita.

Katika kutekeleza azma yake kwa vitendo diwani huyo wa kata ya Gongoni amekuwa akiitumia siku ya Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kupanda miti na kufanya usafi katika kata yake.

Amesema hatua hiyo inalengo la kuongeza kasi ya kupanda miti pamoja na kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ipasavyo na kila mkazi wa kata hiyo.
Abdulrahman ameeleza kuwa kitendo cha kupanda miti mara kwa mara kitasaidia kizazi kinachochipukia kujenga utamaduni wa kuthamini miti ili kuhifadhi na kulinda mazingira.

Diwani huyo amesema suala la ukataji miti kiholela limesababishwa na shughuli za binadamu ikiwemo kuchoma mkaa,kuni, upasuaji mbao, kilimo cha tumbaku na mazao mchanganyiko, ufugaji na ujenzi wa makazi.

Aidha amesema kilimo cha kuhama hama,maarifa madogo ya sayansi ya udongo pamoja na ukosefu wa maarifa ya kilimo cha kisasa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea ukataji wa miti ili kupata maeneo makubwa ya kulima au kufuga.

Abdulrahman amefafanua kuwa licha ya wakulima wengi kulima maeneo makubwa wamekuwa wakivuna kiasi kidogo cha mazao ukilinganisha na muda,nguvu na rasilimali zingine walizotumia.

Diwani huyo wa kata ya Gongoni ameishauri serikali kuwekeza katika matumizi ya nishati mbadala kwa maeneo ya mijini na vijijini, kutoa maarifa chanya ya kilimo na ufugaji bora pamoja na kuhimiza jamii kupanda miti kwa wingi na kuitunza.

Amesema mradi huo wa upandaji miti ameubuni yeye mwenyewe na kwamba atawashirikisha zaidi vijana ili waweze kuwekeza nguvu na maarifa yao katika kutunza mazingira.

No comments: