![]() |
YUSUPH KITUMBO |
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Makamu Mwenyekiti Wakili, Jerome Msemwa
leo imetoa maamuzi ya shauri la upangaji wa matokeo ya kundi C ya Ligi Daraja
la Kwanza (StarTimes League).
Akisoma hukumu hiyo baada ya
kumaliza kuwahoji viongozi wa vilabu na wenyeviti wa vya vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa jana, Wakili Msemwa amesema adhabu hizo zimetolewa kwa kufuata
Kanuni za Nidhamu za TFF, na nafasi ya kukata rufaa kwa wahusika juu ya
maaamuzi hayo ziko wazi.
Klabu za Geita Gold (Geita), JKT
Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) zimekutwa na hatia ya upangaji wa
matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL)
msimu ujao.
Upande wa klabu ya JKT Kanembwa FC
ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL),
baada ya kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C.
Kamati ya Nidhamu imewafungia maisha
kutojihusisha na mpira wa miguu mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v
Geita Gold, Saleh Mang’ola na kamisaa wa mchezo huo Moshi Juma baada ya kukutwa
na hatia ya upagaji matokeo.
Aidha kamati pia imemkuta na hatia
kocha msaidizi wa klabu ya Geita Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha
kutojihusisha na mpira wa miguu.
Magolikipa Mohamed Mohamed wa JKT
Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold wamefungiwa miaka 10 kutojihusisha na
mpira wa miguu sambamba na kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000)
kila mmoja.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold,
Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa
huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa
miguu mkoa wa Tabora, Yusuph Kitumbo, Katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa
wa Tabora, Fateh Remtullah, Mwenyekiti wa klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita na
kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian wamefungiwa maisha kutojihusisha
na mpira wa miguu.
Mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi
Tabora v JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde
wamefungiwa kwa muda wa miaka kumi kutojihusisha na mpira wa miguu, na kutozwa faini
ya shilingi milioni (10,000,000) kumi kila mmoja.
Katibu wa klabu ya Polisi Tabora,
Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa
klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya Polisi
Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya
kutokutwa na hatia.
Kutokana na maamuzi hayo ya Kamati
ya Nidhamu ya TFF, Kamati husika zitakaa kupitia Kanuni na kutangaza timu
itakayopanda Ligi Kuu (VPL) msimu ujao na timu zitakazopanda Ligi Daraja la
Kwanza (StarTimes) msimu ujao.
No comments:
Post a Comment