Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, April 13, 2016

LIGI KUU TANZANIA BARA: "KADI NYEKUNDU NI KWA YANGA TU"




Mechi ya jana ya ligi kuu Soka Tanzania Bara kati ya Yanga na Mwadui FC kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2 kwa 1 na kufikisha pointi 56 kwa michezo 23 ikiwa nyuma ya Simba iliyoko kileleni yenye pointi 57 baada ya kucheza mechi 24.

Mwamuzi wa kati wa mechi hiyo Selemani Kinugani alimtoa kwa kadi nyekundu, Iddi Mobby kunako dakika ya 70 ya mchezo kwa kumchezea rafu kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko.

Mshambuliaji hatari wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma  ameibua mjadala mpya kwa mabeki wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kupata kadi nyekundu.

Ngoma ambaye ameifungia Yanga mabao 14, mpaka sasa kwenye ligi kuu ameweka rekodi mpya ya kuwasababishia mabeki wa kati watatu kadi nyekundu kila alipokutana nao kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika michezo mitatu ya Yanga iliyopigwa kwenye uwanja huo dhidi ya Mbeya City, Simba SC na Kagera Sugar yote ilimalizika kwa timu hizo kuwa na wachezaji pungufu kutokana na kadi nyekundu zilizosababishwa na Ngoma.

Katika mechi yao na Mbeya City, Tumba Sued alipigwa kadi nyekundu baada ya kugongana na Ngoma katika dakika ya 56 na kusababisha pengo kwa timu hiyo ambapo mwisho wa matokeo Yanga ilishinda 3-0.

Mechi Yanga dhidi ya Simba iliyochezwa Februari 21 mwaka huu, kunako dakika ya 24 ya mchezo Mwamuzi wa kati Jonesia Rukyaa alimtoa nje ya dimba  kwa kadi nyekundu beki wa wekundu hao, Abdi Banda kwa kumchezea rafu Ngoma. Katika mechi hiyo Yanga ikashinda kwa magoli 2 kwa bila .

Ngoma kwa mara nyingine alisababisha kwa Kagera Sugar ambapo beki wao, Shaban Ibrahim Sunza, alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuzawadiwa njano mbili kutokana na kumchezea kibabe . Mechi hiyo pia Yanga ilishinda 3-1.

Timu ya Mbeya City imewahi kulalamika kuwa kila inapokutana na Yanga wachezaji wake wamekuwa wakitolewa kwa kadi nyekundu.

Katibu mkuu wa Klabu hiyo Emmanuel Kimbe amewahi kusema timu hiyo katika msimu wao wa kwanza ligi kuu Tanzania Bara 2013/2014 walipokutana na Yanga kadi nyekundu ilikwenda kwa mchezaji wao Steven Mazanda.

Amesema msimu wao wa pili wa 2014/2015 walipokutana na Yanga kadi nyekundu ilienda kwa Them Felix.

Na msimu wao wa tatu wa 2015/2016 wameshuhudia jambo lile lile likijirudia.

No comments: