Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Tuesday, April 12, 2016

WILAYA YA SIKONGE YAZIDI KUPAA KIELIMU


Na Allan Ntana, Sikonge


HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imefanikiwa kuondoa
jinamizi la kufanya vibaya kwenye matokeo ya darasa la 7 baada ya
kushika nafasi ya 7 kitaifa na kuwa miongoni mwa halmashauri 10
bora zilizofanya vizuri sana katika matokeo ya darasa la saba mwaka
jana.

Mkuu wa wilaya hiyo Hanifa Selengu ametoa maelezo hayo hivi karibuni wakati akitoa taarifa ya wilaya kwa mkuu mpya wa mkoa huo Aggrey Mwanri aliyekuwa ziarani wilayani humo.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wilaya hiyo ilikuwa
na matokeo mabaya sana kwa shule za msingi na sekondari kiasi cha
kushika mkia miongoni mwa halmashauri zote hapa nchini.

Amefafanua kuwa baada ya kuchukizwa na hali hiyo waliweka mikakati ya
pamoja kiutendaji ya kuinua kiwango cha elimu na kuongeza ufaulu na
kila mtumishi katika idara ya elimu ya msingi na sekondari kutakiwa
kutekeleza wajibu wake ipasavyo na si vinginevyo.

“Matokeo yake sasa tumeanza kuyaona, kiwango cha elimu kimepanda,
ufaulu wa darasa la saba umeongezeka kutoka 37% kwa mwaka 2011/2012 hadi 75.5% kwa mwaka 2015/2016,” ameongeza.

Amebainisha kuwa jitihada na mshikamano mkubwa kiutendaji miongoni mwa watumishi imewezesha wilaya hiyo kushika namba moja kimkoa katika matokeo ya darasa la 7 kwa miaka miwili  mfululizo yaani 2013/2014 na 2015/2016 sambamba na kushika nafasi ya 7 kitaifa.

Baada ya Halmashauri hiyo kushika nafasi ya 7 kitaifa kati ya
Halmashauri zote 168 hapa nchini, Selengu amesema wilaya yake pia
imepata cheti na tuzo maalumu na imepatiwa fedha taslimu shilingi
244,000,000 kupitia mpango wa Programe for Results ili kuboresha sekta
ya elimu kitaifa.

Aidha Selengu ametaja sifa za wilaya hiyo zilizochochea kupewa
fedha hizo za maendeleo ya sekta ya kielimu kuwa ni uwasilishaji wa
taarifa sahihi na kwa wakati zinapohitajika kitaifa na uingizaji wa
taarifa zilizo sahihi kwenye mfumo wa wizara.

Mengine ni mgawanyo mzuri wa walimu katika shule za msingi na
sekondari kwa kuzingatia ukubwa wa shule na jinsia, ugawaji wa fedha
za ruzuku (Capitation) kwa wakati katika shule, ufuatiliaji mzuri wa
mpango wa elimu bila malipo, ujenzi bora  na imara wa majengo ya shule
bila kupoteza rasilimali na kuongezeka kwa idadi ya walimu kutoka 580
hadi 803.

Aidha amefafanua kuwa mwaka huu 2016 wilaya hiyo imefanikiwa kuandikisha watoto 5841 wa darasa la awali huku watoto 8539 sawa na asilimia 114.9 wakiandikishwa kuanza darasa la kwanza (lengo lilikuwa kuandikisha watoto 7429) na 1535 sawa na asilimia 85.2 wamesajiliwa kuanza kidato cha kwanza.

No comments: