Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Tuesday, May 3, 2016

MKUU WA WILAYA YA SIKONGE AMSWEKA RUMANDE DIWANI WA TUTUO


Na Mwandishi Wetu,Sikonge

MKUU wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Hanifa Selengu amemtupa
rumande diwani wa kata ya Tutuo kupitia CHADEMA Elemence Msumeno akimtuhumu kumdhalilisha kwa kuhoji utaratibu wa uteuzi wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa JKT.

Tukio hilo limetokea kwenye kikao cha baraza la madiwani siku ya
Ijumaa ya mwezi April 29 mwaka huu baada ya diwani huyo alimuhoji
mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Peter Nzalalila kuhusu vigezo vilivyotumika kuteua vijana waliojiunga na mafunzo ya JKT.

Msumeno alisema kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika utekelezaji wa zoezi hilo kwa kuonyesha  dalili za upendeleo kwa vijana  ambao wamechaguliwa na kwamba wengi wao si wakazi wa wilaya ya Sikonge wametoka Dodoma,Zanzibar na Morogoro.

Diwani huyo amesema katika zoezi hilo ni vijana wawili tu ambao wamechaguliwa kutoka Sikonge na kwamba kuna ubinafsi umefanyika ikiwemo watumishi wilayani humo kutumia nafasi zao kupitisha ndugu zao.

Amesema vijana waliochaguliwa wengi wao hawana sifa huku vijana wengi sifa wakiachwa na niwakazi wa wilaya ya Sikonge.


Baada ya diwani huyo kutoa hoja hiyo mkuu wa wilaya Hanifa Selengu alitoa ufafanuzi wake kuwa vijana waliochaguliwa ni kweli wengi wao wametoka nje ya wilaya yake lakini wameombea nafasi hizo wilaya ya Sikonge.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya hakuridhika na swali hilo hivyo alitoka
nje kwa jazba na alimuita kaimu kamanda wa polisi wilaya Mayala Magesa na kumuagiza amkamate diwani amuweke ndani.

Msumeno alitolewa nje na OCD msaidizi na kuelezwa kuwa mkuu wa wilaya ameagiza awekwe ndani kwa saa 48 hivyo na kumtaka waandamane kwenda kituo cha polisi mnamo majira ya saa 12:09 jioni.

Hata hivyo mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Sikonge ambaye pia ni diwani wa kata ya Ngoywa Lucas Kibelenge alihoji mamlaka ya mkuu wa wilaya kutoa amri ya kukamatwa diwani anayehoji mambo yanayowahusu wananchi wake.
 

Baada ya kutoka rumande majira ya saa 07:34 mchana siku ya Jumapili Msumeno alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa kitendo cha mkuu wa wilaya kumtupa ndani ni udhalilishaji hivyo anakusudia kuongea na mwanasheria wake ili kuchukua hatua za kisheria.

No comments: