Na, Thomas Murugwa,Tabora.
Mkuu wa kitengo cha biashara cha
kampuni ya simu za mkononi mtandao wa Hallotel Hoang Vanch Linh (36)
maarufu kwa jina la “Peter” amekamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU kwa tuhuma za kuomba
na kupokea rushwa.
Akizungumza na waandishi wa
habari kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Tabora Fidelis Kalungura amesema
raia huyo wa Vietnam alikamatwa Aprili 08 mwaka huu baada ya maofisa
wake kupewa taarifa na kisha kuweka mtego uliomnasa.
Kamanda Kalungura amesema kuwa raia
huyo wa Vietnam alikamatwa akipokea rushwa ya shilingi laki tano ikiwa ni
sehemu ya malipo ya shilingi milioni 1.5 alizoomba kutoka kampuni ya ulinzi
iitwayo State.
Amebainisha kuwa TAKUKURU ilipewa
taarifa kuwa mkuu huyo wa kitengo cha biashara Hallotel aliomba apewe fedha
hizo toka kwenye kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kulinda minara ya simu
ili waendelee kupewa mkataba wa kazi hiyo.
Kalungura amesema kwamba mara
baada ya kukamatwa na kuhojiwa Mvietinam huyo alikana na alipewa dhamana
wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Kamanda Kalungura amebainisha kuwa
bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na endapo ikibainika kama
aliomba na kupokea fedha hizo kama hongo atafikishwa mahakamani .
No comments:
Post a Comment