Na Paul Christian, Tabora.
Imebainika kuwa baadhi ya viongozi wa dini mkoani
Tabora wamekuwa wakifungisha ndoa pasipo kuhakiki vipimo vya afya vya wanandoa
husika ili kuepuka kuambukizana magonjwa mbalimbali.
Uchunguzi uliofanywa na VOT FM STEREO katika
Maabara kadhaa mjini Tabora umebaini kuwa baadhi ya shughuli za ndoa zimekuwa
zikifunjika katika hatua za mwisho kabla ya Ndoa kufungwa baada ya ndugu wa mmoja wa
wanandoa kupata taarifa zenye utata kuhusu afya ya mmoja wa wanandoa na hivyo
kulazimisha wakafanyiwe vipimo.
Akizungumzia hali hiyo mmoja wa watoa huduma za Maabara ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema wamekuwa wakipokea kesi
nyingi za wachumba waliokuwa kwenye hatua ya kufunga ndoa na kulazimika kufanya
vipimo vya afya kwa lengo la kuhakiki uvumi unaomuhusu mmoja wa wachumba hao.
Amesema, “tunapochukua sampuli ya damu katika
mazingira hayo na kwenda kupima mara nyingi tumekuwa tukigundua kuwa mmoja wa
wachumba hao anaishi na virusi vya UKIMWI hali ambayo inapelekea uchumba
kuvunjika katika hatua za mwisho.”
Mtaalamu huyo amefafanua kuwa hali hiyo ya fedheha,aibu
na inayosababisha upotevu wa fedha na muda inaweza kuepukwa kama watu walioko
kwenye uchumba wakijenga utamaduni wa kupima afya zao mapema.
Aidha amesisitiza viongozi wa dini kuacha tabia ya
kufungisha ndoa kwa mazoea na badala yake wahakikishe wahusika wamefanyiwa vipimo
vya afya na kukubaliana kwa dhati hata kama mmoja wao anaishi na virusi vya
UKIMWI.
Afisa huyo ameshauri madhehebu ya dini kuwahimiza
waumini wao walioko kwenye uchumba wa asili kufanyiwa vipimo vya virusi vya
ukimwi, ujauzito,kaswende,seli mundu (sickle cell) na homa ya Ini kwa lengo la
kuepuka matatizo kwenye ndoa.
Amesema, “Baadhi ya wanawake wamekuwa wakifunga
ndoa wakiwa na ujauzito usiohusiana na ndoa yenyewe, kwa maana ya ujauzito wa
mwanaume mwingine jambo ambalo ni hatari.”
Mtaalam huyo wa maabara ametoa mfano wa baadhi ya
wanawake ambao wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa waume au wachumba wao kwa
kwenda maabara na mashoga zao wenye mimba ambao utoa haja ndogo kwa niaba ya
hao wadanganyifu na kufanyiwa vipimo vya ujauzito.
Amesema hali hiyo ya kitapeli inaweza kukomeshwa
endapo wanaume watajenga mazoea ya kwenda na wenzi wao kwenye maabara wakati wa
kufanyiwa vipimo muhimu kama vya ujauzito.
No comments:
Post a Comment