
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Tabora
imebaini uwepo wa mianya ya rushwa kwenye Machinjio na Soko kuu yanayosimamiwa
na halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Tabora Fidelis
Kalungura amesema katika machinjio ya mjini Tabora taasisi hiyo iligundua
ongezeko la viwango vya ushuru kwa shilingi 500 kwa kila ng’ombe anayehifadhiwa
kwa siku zisizo za kazi.
Amesema pamoja na kutoza ushuru huo wenye maofisa wa halmashauri
wanaosimamia machinjio hiyo wamekuwa hawatoi stakabadhi kwa wamiliki wa ng’ombe
hao.
Kalungura amebainisha kuwa fedha hizo zinazokusanywa kupitia
ushuru huo ambao hautolewi stakabadhi zimekuwa zikitumika kuwalipa malipo ya
ziada watumishi hao wa umma.
Aidha amefafanua kwa mujibu wa sheria za nchi jukumu la kuwalipa
malipo ya ziada watumishi hao ni la mwajiri wao ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Kalungura amesema eneo jingine lililobainika kuwa na mianya ya
rushwa ni ukarabati mdogo wa machinjio hiyo ambao haukulingana na thamani ya halisi
ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Tabora amesema mwanya mwingine wa
rushwa katika machinjio hiyo upo kwenye usimamizi wa Sheria, Kanuni na taratibu
kwa kuruhusu magari yasiyo na ubora kubeba nyama kwenda kwa walaji.
Amebainisha kuwa katika eneo hilo kutokana na udhaifu wa usimamizi wa sheria
baiskeli na pikipiki zimeruhusiwa kusafirisha nyama jambo ambalo ni kinyume cha
sheria.
Kalungura amesema taasisi hiyo imebaini mianya ya rushwa kwenye
Soko kuu la mjini Tabora kwa kutofahamika idadi ya walipa ushuru kwa kuwa idadi
kamili ya vizimba haipowazi.
Aidha ameeleza katika soko hilo kunaukiukwaji wa sheria,kanuni
na taratibu kwa kuwa ushuru haulipwi kwa wakati na hakuna hatua zozote
zinazochukuliwa.
Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema taasisi yake imebaini kuwa
wakusanya ushuru hawalipwi posho zao za kazi za ziada kwa wakati na wanaidai
halmashauri ya Manispaa ya Tabora jambo ambalo linatoaushawishi wa kupokea
rushwa.
Kalungura amebainisha katika soko hilo hakuna mfumo unaokubalika
katika utunzaji wa kumbukumbu na ufuatiliaji pia hakuna ushirikishwaji wa
wafanyabiashara katika kufanya maamuzi mbalimbali yanayowahusu.
Ameeleza kuwa wakusanya ushuru hao wanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi hawana kompyuta kwa ajili ya kutunzia kumbukumbu wala vyombo vya usafiri kama baiskeli na pikipiki.
Hata hivyo taasisi hiyo imeiagiza halmashauri ya manispaa ya
Tabora kuchukua hatua za kuziba mianya hiyo ya rushwa katika Machinjio na Soko
Kuu mjini Tabora.
No comments:
Post a Comment