Na
Hastin Liumba,Tabora
Diwani
wa kata ya Gongoni manispaa ya Tabora Kessy Sharrif Abdulrahman amewaasa wakazi
wa kata hiyo na maeneo mengine kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa
kupanda miti.
Amesema
suala la kupanda miti linapaswa kuwa ajenda ya kudumu kwa wakazi wa mkoa wa
Tabora ambao kwa sasa umeanza kuathiriwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira
ikiwemo ukataji miti kwa matumizi mbalimbali.
Abdulrahman
amebainisha kuwa maeneo ya mkoa wa Tabora kwa sasa yameanza kukabiliwa na uhaba
wa mvua na ongezeko la joto tofauti na miaka iliyopita.
Katika
kutekeleza azma yake kwa vitendo diwani huyo wa kata ya Gongoni amekuwa
akiitumia siku ya Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kupanda miti na kufanya
usafi katika kata yake.
Amesema
hatua hiyo inalengo la kuongeza kasi ya kupanda miti pamoja na kuhakikisha miti
hiyo inatunzwa ipasavyo na kila mkazi wa kata hiyo.
Abdulrahman
ameeleza kuwa kitendo cha kupanda miti mara kwa mara kitasaidia kizazi
kinachochipukia kujenga utamaduni wa kuthamini miti ili kuhifadhi na kulinda
mazingira.
Diwani
huyo amesema suala la ukataji miti kiholela limesababishwa na shughuli za
binadamu ikiwemo kuchoma mkaa,kuni, upasuaji mbao, kilimo cha tumbaku na mazao
mchanganyiko, ufugaji na ujenzi wa makazi.
Aidha
amesema kilimo cha kuhama hama,maarifa madogo ya sayansi ya udongo pamoja na
ukosefu wa maarifa ya kilimo cha kisasa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea
ukataji wa miti ili kupata maeneo makubwa ya kulima au kufuga.
Abdulrahman
amefafanua kuwa licha ya wakulima wengi kulima maeneo makubwa wamekuwa wakivuna
kiasi kidogo cha mazao ukilinganisha na muda,nguvu na rasilimali zingine
walizotumia.
Diwani
huyo wa kata ya Gongoni ameishauri serikali kuwekeza katika matumizi ya nishati
mbadala kwa maeneo ya mijini na vijijini, kutoa maarifa chanya ya kilimo na
ufugaji bora pamoja na kuhimiza jamii kupanda miti kwa wingi na kuitunza.
Amesema
mradi huo wa upandaji miti ameubuni yeye mwenyewe na kwamba atawashirikisha
zaidi vijana ili waweze kuwekeza nguvu na maarifa yao katika kutunza mazingira.