Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, December 30, 2015

WAZIRI MKUU ANUSA UFISADI KIGOMA



 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu ya tuhuma ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.

“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

“Nataka kujua nani alifanya tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua hatua za kinidhamu,” alisema.

Viongozi walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng. Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.

Kuhusu uuzwaji wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst), Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015 akitaka viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na mchakato huo usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja pekee.

 Tuhuma nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).

Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.

Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na Mhasibu Mkoko.

Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 30, 2015.





Monday, December 28, 2015

SIMBA WAVAMIA MAKAZI NA KUUA NG'OMBE WANNE WILAYA YA UYUI MKOANI TABORA.




Na Paul Christian,Tabora.

Simba wanyama wamevamia makazi ya watu na kuua ng’ombe wanne katika vijiji vya Nkulusi na Ndono katika kata ya Ndono wilaya ya Uyui mkoani Tabora.

Akizungumza kwa njia ya simu leo mchana mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Said Ntahondi amesema simba hao wamewaua ng’ombe wawili katika kijiji cha Nkulusi usiku wa Jumamosi na usiku wa Jumapili wamewaua ng’ombe wengine wawili katika kijiji cha Ndono.

Amesema mnamo majira ya saa tisa alasiri leo simba hao wameonekana katika milima ya Mbola iliyopo kata ya Isila, tarafa ya Ilolangulu wilayani humo na hivyo kuwataka wakazi wa tarafa hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya simba hao.

Ntahondi ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbali mbali ikiwemo askari wa wanyama pori kufanya msako dhidi ya simba hao kwa lengo la kuzuia madhara zaidi yanayoweza kutokea kwa binadamu na mifugo.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri amewataka wakazi wa kata zote za tarafa ya Ilolangulu kutembea kwa kujihami kwa kuwa na silaha za jadi kama vile mashoka, mapanga, mikuki,pinde na mishale tayari kukabiliana na wanyama hao.

Aidha Ntahondi amewataka wazazi na walezi kuwaangalia watoto wao na kuchukua tahadhari kila mahali wanapokuwa katika kipindi hiki ambacho simba hao wanatafutwa.

Amefafanua kuwa wataalamu wa wanyapori wameeleza kuwa simba wanatabia ya kutembea hadi umbali wa kilometa 50 katika uelekeo wowote kutoka mahali walipo hivyo ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari.

Ntahondi amewataka wanachi kutoa taarifa mara moja kwa watendaji wa vijiji na kata, mkuu wa wilaya ya Uyui, mwenyekiti wa halmashauri na hata kwa viongozi wengine endapo watawaona simba hao ili hatua zichukuliwe.  


WAFANYABIASHARA WACHANGIA UKARABATI KITUO CHA POLISI



Na Elias Shija, Uyui.
 
Wafanyabiashara wa kata ya Bukumbi wilaya ya Uyui mkoani Tabora wamechanga kiasi cha Tsh. 3,400,000/= kwa ajili ya kukarabati jengo la kituo kidogo cha polisi cha kata hiyo.

Akizungumzia suala hilo katibu wa umoja wa wafanyabiashara hao Maziku Kanati amesema fedha hizo zimetumika kukarabati jengo hilo ili kuimarisha ulinzi katika kukabiliana na matukio ya mara kwa mara ya uhalifu katani humo.

Amesema ongezeko la matukio ya uhalifu dhidi ya watu na mali zao yamepelekea wafanyabiashara hao kujitoa kwa hali na mali kukarabati jengo hilo ili liwe na sifa zinazokubalika na kuwawezesha polisi kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Kanati amebainisha kuwa hali hiyo itawasaidia kudumisha amani na utulivu wakati wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kijamii na uzalishaji mali.

Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Jonas Mheza amesema kuimarika kwa kituo hicho cha polisi kutasaidia kuongezeka kwa askari wanaotoa huduma katika maeneo yao.

Aidha amesema matukio ya kihalifu katani humo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hali inayowasababisha baadhi ya wafanyabiashara kuwa na hofu kufanya uwekezaji wenye tija.

Mwenyekiti huyo amewataka wafanyabiashara na wananchi wa kata ya Bukumbi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi katika kuwafichua wahalifu ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamemuomba kamanda wa polisi mkoa wa Tabora kuwaondoa askari waliowahi kufanya kazi katika kituo hicho siku za nyuma kwa kuwa hawana rekodi ya uadilifu katika kutekeleza majukumu yao.

Saturday, December 26, 2015

HOSPITALI YA KITETE YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA DAWA ZA KIFAFA




Na, Rehema Cleophace,Tabora.
  
Idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa kifafa na kupelekwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Tabora Kitete inaendelea kuongezeka kuliko magonjwa mengine ya akili mkoani hapa.

Afisa muuguzi msaidizi wa magonjwa ya akili katika hospitali ya Kitete bibi Suzan Msagata amesema idadi ya wagonjwa hao imeongezeka mara mbili kwa mwaka huu kutokana na upungufu wa dawa za ugonjwa huo unaoikabili hospitali hiyo.

Amesema hali ya upungufu wa dawa unasababisha idadi ya wagonjwa kuongezeka kutokana na kutopatiwa matibabu ya kutosha na hali ya kuumwa kujirudia.

Afisa muuguzi huyo amesema mwaka huu zaidi ya wagonjwa 600 wametibiwa katika hospitali hiyo na kuruhusiwa na kwamba waliolazwa kwa mwaka huu ni wagonjwa 30.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kitengo hicho cha magonjwa ya akili bibi Msagata amesema tatizo la kukosekana dawa limekuwa sugu hivyo ameitaka serikali kuhakikisha inatoa dawa za kutosha ili wagonjwa watibiwe kwa kupewa dawa za muda mrefu kwa lengo la kuepuka ugonjwa kujirudia rudia.

Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni jamii kuuhusisha ugonjwa wa kifafa na imani za kishirikina hali inayosababisha wagonjwa kuongezeka kutokana na wengi wao kuamini kuwa mgonjwa wao karogwa hivyo kuchukua uamuzi wa kumpeleka kwa mganga wa kienyeji.

Kutokana na hali hiyo muuguzi huyo msaidizi amewasihi wananchi kuachana na imani hiyo badala yake wawapeleke wagonjwa wa kifafa hospitalini kwa matibabu ambayo hutolewa bure.

KANISA LA KCC TABORA LAMPONGEZA RAIS DKT. MAGUFULI

Na Allan Ntana, Tabora

KANISA la Kitete Christian Center (KCC-TAG) la mjini Tabora
limempongeza Rais wa awamu ya tano Dkt.John Pombe Magufuli kwa hatua mbalimbali za kiutendaji alizochukua kulinda maslahi ya Taifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Askofu Paul Meivukie wa kanisa hilo
alipokuwa akitoa salamu za Krismasi mara tu baada ya kumalizika kwa
ibada iliyofanyika kanisani hapo.

Alisema utendaji kazi wa Rais Magufuli unapaswa kuungwa mkono na wapenda maendeleo wote kwani ameonyesha dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya taifa kwanza pasipo kuangalia itikadi za kisiasa.

“Rais ameonyesha wazi dhamira yake ya kuleta maendeleo na kile
anachotaka kifanyike anakisimamia kwa vitendo, katika hili
tunampongeza sana na tutaendelea kumwombea awe na afya njema na
hekima katika utendaji wake”, aliongeza.

Aidha Askofu Meivukie alipongeza uamuzi wa Rais wa kufanya maadhimisho ya mwaka huu ya Uhuru wa Tanganyika kuwa siku ya usafi wa mazingira kwa nchi nzima huku akibainisha kuwa usafi ni jambo la muhimu sana kwa ustawi wa jamii na linapaswa kuendelezwa na watendaji wote.

Ili kudumisha amani, upendo na mshikamano katika nchi hii, Askofu
alitoa wito kwa Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano kushughulikia
changamoto kadhaa zilizopo ikiwemo suala la uchaguzi wa Zanzibar ili
lisije kuondoa amani iliyopo sasa hapa nchini.


‘Tunapoadhimisha sikukuu hii ya kuzaliwa kwa Yesu Kristu kila mmoja
anapaswa kujichunguza na kujiwekea tumaini jipya la kuingia 2016 akiwa
na Bwana Yesu, hivyo natoa wito kwa Watanzania wote kuendelea
kudumisha amani, upendo na mshikamano’, aliongeza.

Akitoa salamu kwa niaba ya waumini, Mzee  wa kanisani kiongozi Dr. Frank Matimbwa aliwataka Watanzania wote kumpokea Yesu Kristu katika maisha yao kwa kuwa ni mkombozi wa ulimwengu,mfalme wa amani na mshauri wa ajabu.

Aliongeza kuwa Yesu Kristu aliyezaliwa ndiye atakayetungooza kulinda
na kutetea amani tuliyonayo sasa hivi ili kuendeleza ustawi wa kanisa
na nchi kwa ujumla.