Na Thomas Murugwa,Igunga.
Viongozi watano wa serikali ya kijiji cha
Igogo wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamefikishwa mahakama ya Wilaya hiyo
wakikabiliwa na mashitaka manne ya kuhujumu uchumi.
Viongozi hao waliopandishwa kizimbani ni mwenyekiti
wa kijiji hicho Elinkaila Issa, afisa mtendaji Henry Luhende Masanja, wajumbe
wa kamati ya fedha Helena Maduluma na Boniphace Jagadi pamoja na mtunza
hazina Emanuel Simon.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Edsoni
Mapalala wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ulidai
mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Igunga Ajali Milanzi kuwa
watuhumiwa walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 13 na Novemba 24, 2014.
Katika shitaka la kwanza ilidaiwa kuwa tarehe 13 Oktoba
2014 watuhumiwa kwa kutumia nyadhifa zao waliiba shilingi 5,100,000/- fedha za
shule ya msingi Igogo.
Wakili mapalala alisema kuwa watuhumiwa kwa
kutumia nyadhifa zao vibaya waliiba kiasi hicho cha fedha ambazo zilikuwa
zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa matundu 12 ya vyoo vya shule ya
msingi Igogo.
Ilidaiwa katika shitaka la pili na wakili
Mapalala kuwa tarehe 24 Novemba 2014 watuhumiwa kwa pamoja waliiba shilingi
3,120,00/- zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa
choo cha ofisi ya serikali ya kijiji hicho.
Katika shitaka la tatu ilidaiwa na upande wa
mashitaka kuwa watuhumiwa kwa pamoja na kwa makusudi wakiwa viongozi wa kamati ya fedha ya serikali ya
kijiji hicho walijitwalia jumla ya shilingi 8,220,000/- na kusababisha ujenzi
wa matundu ya vyoo kutojengwa.
Wakili Mapalala alidai katika shitaka la nne kuwa kutokana na kitendo
hicho watuhumiwa waliisababishia halmashauri ya wilaya ya Igunga hasara
ya shilingi 8,220,000/=.
Watuhumiwa wote wamekana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana hadi
julai 12 mwaka huu shauri hilo litakapoanza usikilizwaji wa awali kwani upelelezi
wake umekamilika.
No comments:
Post a Comment