Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, July 25, 2016

TANESCO: "FOMU ZA MAOMBI YA KUUNGANISHIWA HUDUMA YA UMEME HAZIUZWI"



Na Paul Christian,Tabora.

Shirika la ugavi wa umeme TANESCO mkoa wa Tabora limesema fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma ya umeme kwa wananchi zinatolewa bure kwenye ofisi za shirika hilo ngazi ya wilaya na makao makuu ya mkoa.

Kaimu meneja wa shirika hilo mkoa wa Tabora injinia Melkiad Msigwa ametoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu wilaya ya Kaliua kudai kutozwa kati ya shilingi 30,000/- na 50,000/- na watu wanajiita mafundi wa umeme ili kupata fomu hizo.

Malalamiko hayo ya wananchi yametolewa hivi karibuni wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Ulyankulu John Peter Kadutu alipofanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji ya mradi wa usambazaji umeme vijijini ambapo alizungumza na wananchi katika vijiji vya Ibambo,Usigala, Makonge,Mkindo,Kaswa, Taba,Sasu na Kashishi jimboni humo.

Akijibu malalamiko hayo ya wananchi Kaimu meneja huyo wa TANESCO amebainisha kuwa fomu hizo hazipaswi kuuzwa zinatolewa bure na kwamba akitokea mtu anafanya ushawishi wa udanganyifu ili ajipatie fedha akamatwe na achukuliwe hatua za kisheria.

Injia Msigwa amewataka wananchi walioko kwenye vijiji vilivyounganishwa na mtandao wa umeme kupitia mradi wa Usambaji umeme vijijini REA awamu ya pili kuzitumia ofisi za TANESCO kwenye wilaya au kufika makao ya mkoa ya shirika mjini Tabora ili kupata fomu hizo pamoja na taarifa nyingine muhimu.

Aidha amewataka wananchi hao kuwatumia wataalamu kutoka kwenye makampuni yaliyosajiliwa na ambayo yanatambuliwa na TANESCO katika kufanya utandazaji wa miundombinu ya umeme kwenye nyumba na maeneo ya biashara.

Injia Msigwa ametoa onyo kwa watu wanaotumia fursa ya umeme vijijini kujinufaisha kwa udanganyifu kwa kufanya kazi za umeme majumbani pasipo vibali vya serikali kwamba watachuliwa hatua.

Kaimu meneja huyo wa TANESCO mkoa wa Tabora amewataka wananchi, viongozi wa serikali za vijiji na kata ambazo zimepitiwa na umeme kuchukua tahadhari kwa kufika ofisi za TANESCO kupata orodha ya makampuni ambayo yanatambuliwa kisheria, na hivyo kuwa na sifa ya kuwahudumia watu vijijini.


No comments: