Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, July 25, 2016

WAKAZI WA TABORA WAJIUNGE NA MIFUKO YA BIMA YA AFYA



Na Paul Christian,Tabora.

Wakazi wa mkoa wa Tabora wameaswa kujiunga na mifuko ya bima ya afya ambayo itawasaidia kuwa na uhakika wa matibabu.

Rai hiyo imetolewa na Meneja wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF mkoa wa Tabora Vedastus Kalungwani katika mahojiano maalum na waandishi wa habari yaliyofanyika ofisini kwake.

Amesema mifuko ya bima ya afya inamanufaa mbalimbali kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa kununua dawa na vifaa tiba.

Kalungwani amebainisha kuwa hadi sasa takwimu zinaonesha kuna mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unahudumia wakazi wa halmashauri za vijijini pamoja na Tiba kwa Kadi (TIKA) inayohudumia wakazi wa mjini.

Meneja huyo amesema wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa kujiunga na mifuko hiyo na kwamba waachane kutibiwa kwa mazoea jambo ambalo linahatarisha uhai wao kwa kuwa magonjwa hayapigi hodi.

Kalungwani amesema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Tabora umejiwekea mikakati ya kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko hiyo kwa kuzifikia halmashauri zote za mkoa wa Tabora.

Meneja huyo wa NHIF mkoa wa Tabora amefafanua kuwa katika mikakati waliojiwekea ni pamoja na kupanua wigo wa huduma kwa kuanzisha mpango wa matibabu kwa wajasiriamali (KIKOA) ambao umelenga vikundi vya waendesha bodaboda, wakulima wa tumbaku pamoja na wajasiriamali wengine kwa kulipia shilingi 76,800/- kwa mwaka ambayo itamuwezesha kutibiwa mahali popote nchini.

Kalungwani amebainisha kuwa katika kuwafikia wajasiriamali hao wamejiwekea lengo la kuvifikia vikundi 990 katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza mkakati wa mwaka huu wa fedha wameweka mpango wa huduma ya afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano unajulikana, “Toto Afya Kadi” kwa gharama ya shilingi 50,400/- kwa mwaka.

Aidha Kalungwani ametaja baadhi ya sababu zinazowakatisha tamaa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya kuwa ni pamoja na huduma duni kwenye zahanati na vituo vya afya, idadi ndogo ya wahudumu wa afya,kauli chafu kwa wagonjwa, ukosefu wa dawa na vifaa tiba.

Meneja huyo wa NHIF mkoa wa Tabora ametoa wito kwa wahudumu wa afya kutoa huduma kwa misingi ya viapo vyao vya kazi, maadili ya utumishi na kwa misingi ya weledi wa kitaaluma ili kuwafanya wananchi kuwa na imani ya kupona kwa matibabu wanayotoa.






No comments: