Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, July 13, 2016

WANAWAKE MKOANI TABORA WAHIMIZWA KULIPA KODI



Na Paul Christian, Tabora.

Wanawake wa mkoa wa Tabora wamehimizwa kulipa kodi kupitia shughuli zao za ujasiriamali ili kuisaidia serikali kutekeleza kwa ufanisi miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT mkoa wa Tabora ambaye pia mbunge wa viti maalum Mwanne Mchemba wakati akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Umoja huo wa wilaya ya Uyui kwenye kikao kilichofanyika mjini Tabora.

“Na sisi wenyewe kama wanaCCM miongoni mwetu waliokuwepo wasiotaka kulipa kodi uongo, kweli? Sasa mtapataje maendeleo kama hamtaki kulipa kodi.” Alihoji mwenyekiti huyo.

Mwanne amewataka wanawake hao kwenda kwenye maeneo yao kuhimiza wanawake wenzao na jamii kwa ujumla kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa kila shughuli kiuchumi wanazozifanya.

Mwenyekiti huyo wa UWT amesema wanawake hao wanapaswa kudai risiti kila mara wanapofanya manunuzi kwa wafanyabiashara ambao biashara zao ni rasmi na zinatambulika kwa kuwa kwa kufanya hivyo wataiingizia mapato serikali.

Aidha amesema, “kama kuna miradi inakwenda ovyo ni vyema kutoa taarifa kwa diwani wa kata au madiwani wa viti maalum ili wachukue hatua dhidi ya uchakachuaji katika mradi husika.”

Mwanne amebainisha kuwa serikali ya awamu ya Tano imajipambua kwa kupambana na mchwa walikuwa wakiitafuna miradi ya maendeleo kwa wizi na ubadhirifu.

Akitoa salamu kwa  baraza hilo mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa ambaye pia mbunge wa viti maalum mkoa wa Tabora Munde Tambwe amesema wanawake wanapwa kuwa wamoja na kuacha tabia ya kubaguana katika shughuli za kiuchumi.

“Ili kujenga UWT yenye nguvu tunapaswa kuondoa matabaka na hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi ambao ulikuwa na heka heka za hapa na pale na hata kubadilishana maneno.”amesema Munde.

Munde amesema kazi kubwa watakayoifanya wabunge wa viti maalum mkoa wa Tabora ni kuchochea maendeleo kwa wanawake wote pasipo kuwabagua kwa misingi ya itikadi zao.

Amesema, “Sisi ni chama tawala, tufanye kazi ya kuleta maendeleo kwa akinamama wa CCM pamoja na wale wasio kuwa wa CCM, tusiwabague, tusiwatenge katika shughuli za maendeleo, tuwakaribisha tuwasogeze.”

Awali katibu wa CCM mkoa wa Tabora Janat  Kayanda aliwapongeza wanawake hao kwa namna walivyokisaidia Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi katika majimbo mawili ya ubunge na kata nyingi wilayani Uyui.
Mwisho.



No comments: