Na Paul Christian,Tabora.
Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS) mkoa wa Tabora wamepongezwa kwa kutengeneza barabara yenye
urefu wa kilometa 46.6 kutoka Ulyankulu hadi Ng’wande ambayo ilikuwa haipitiki
wakati wa mvua za masika.
Akiwahutubia wakazi wa
vijiji vya Taba,Sasu na Kashishi vilivyopo wilaya ya Kaliua Mbunge wa Jimbo la
Ulyankulu John Peter Kadutu alisema TANROADS mkoa wa Tabora wamefanya kazi nzuri
iliyorudisha matumaini ya wakazi hao kuweza kuyafikia maeneo mengine.
Alisema, “Barabara hii
ni uti wa mgongo wa mawasiliano ya kiuchumi kati ya wakazi wa jimbo la
Ulyankulu upande wa mkoa wa Tabora pamoja na Ushetu na Kahama kwa upande wa
mkoa wa Shinyanga.”
Kadutu alifafanua kuwa
TANROADS pia wamepanga kuimarisha barabara ya kutoka Makazi kupitia Uyowa hadi
makao makuu ya wilaya, Kaliua ambapo hakukuwa na barabara ya uhakika
kuunganisha maeneo hayo.
Akizungumzia barabara
hiyo mmoja wa wakazi wa kijiji cha Taba Yudita Sayumwa alishauri, “Wataalam wa TANROADS wanapaswa
kuwauliza wenyeji kuhusu maeneo korofi ambayo hukatika wakati wa mvua ili
yafanyiwe matengenezo ya uhakika tofauti na ilivyosasa.”
Kaimu afisa mtendaji
wa kijiji cha Sasu Samwel Gogoja Ngokolo naye alitoa ushauri kwa meneja wa TANROADS
mkoa wa Tabora kuhusisha serikali za vijiji ili kubaini maeneo korofi pamoja na
kuweka matuta kudhibiti mwendokasi wa magari eneo la shule ya msingi kijijini
humo.
Kwa upande wake mwenyekiti
wa serikali ya kijiji cha Kagera kata ya Kashishi jimboni humo Dennis Steven
Mkindo alitaka ufafanuzi kuhusu baadhi ya matengenezo katika barabara hiyo
kuonekana dhaifu kwa kuwa haijawekwa molamu.
Akijibu hoja hizo mhandisi
wa TANROADS mkoa wa Tabora anayeshughulikia barabara za mkoani humo Siperi Kato
alisema, “kazi ya kujenga karavati bado inaendelea na mkandarasi bado
hajamaliza kazi.”
Alibainisha kuwa
mkandarasi huyo bado anayomakaravati karibu ya 100 na kwamba amekuwa akiyaanda
kwa ajili ya kudhibiti maeneo korofi katika barabara hiyo.
Mhandisi Kato
aliongeza, “TANROADS kwa kushirikiana na mkandarasi kampuni ya SAMOTA
watahusisha viongozi wa serikali za vijiji hivyo ili kubaini maeneo
yanayohitaji matengenezo ya ziada kutoka na uzoefu wao.”
Mhandisi huyo alitoa
ushauri kwa wakazi wa vijiji hivyo kuzingitia umbali wa hifadhi ya barabara kwa
kupima mita 30 kutoka katikati ili kujenga makazi au maeneo ya biashara kwa
kuwa imepandishwa hadhi na kuwa ya mkoa tofauti na zamani.
No comments:
Post a Comment