Na
Paul Christian,Tabora
Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani Tabora
zimeagizwa kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha
vijana katika maeneo yao.
Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa agizo
hilo jana alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya kutambua fursa za ajira kwa
vijana 191 wa wilaya ya Uyui yaliyofanyika katika chuo cha kilimo Tumbi katika
manispaa ya Tabora.
“Ninaanza kucheck mahesabu ya halmashauri zote za
mkoa wa Tabora na nikibaini halmashauri ambayo haijatenga asilimia tano kwa
ajili ya vijana hatutapitisha bajeti ya halmashauri husika,” amesema.
Mwanri amesisitiza kuwa suala la kutenga asilimia
tano ya mapato ya ndani ya halmashauri hizo ni la kisheria na kwamba halina
mjadala.
Aidha amezitaka halmashauri hizo kuweka vipaumbele
madhubuti katika mipango yao ili ziweze kuondoa vikwazo vinavyoweza
kuwakwamisha vijana kujichukulia fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Halmashauri zinapaswa kuweka vipaumbele katika
kuchimba mabwawa, kutengeneza miundombinu ya barabara pamoja na mambo mengine
kwa lengo la kuwafanya vijana wanaojiajiri wayafikie masoko na kutoa huduma
mbalimbali za kibiashara.”Amesema Mwanri.
Mkuu huyo wa mkoa amezitaka halmashauri hizo
kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana ili wawe wabunifu wa kujiajiri na kutoa
ajira kwa watu wengine.
Akitoa rai kwa vijana hao amesema wanapaswa
kubadili mtazamo wa kutaka kuajiriwa na badala yake wafikirie kuwa waajiri wa
wale wanaofikiria kuhitimu masomo na kuajiriwa.
Awali kiongozi wa shirika la Millenium Promise
Tanzania Dkt. Gerson Nyadzi amesema mafunzo hayo yanatokana na mradi
unaojulikana Opportunities for Youth Employment (OYE).
“Vijana hawa wamejifunza nini maana ya mawasiliano,kuwa
na nia au malengo katika maisha yao,kuweka kumbukumbu na kuhesabu,namna ya kupunguza
msongo (stress management) pamoja na mawasiliano na utambuzi wa fursa.” Amesema.
Amesema mafunzo hayo ni ya awali yanayojulikana kama
“stadi za kijamii” na hatua itakayofuata itakuwa ni kufundishwa masuala ya
utaalam au ufundi (technical skills training).
Nyadzi amebainisha kuwa katika mafunzo hayo ya
awali vijana hao wamejifunza kwa kujigawa katika makundi makuu matatu ikiwemo
kilimo cha bustani,ufugaji wa kuku na nyuki.
Ameyataja makundi mengine kuwa ni kutafuta nishati
mbadala (renewable energy) ambapo watafanya biogas na utengenezaji wa majiko
banifu pamoja na kundi la usafi wa mazingira na maji ( water sanitation and
hygiene).
Dkt. Nyadzi amesema vijana hao wenye umri wa kati
ya miaka 18 na 30 wanatoka katika kata za Magiri,Ilolangulu,Kigwa,Isila na
Isikizya katika wilaya ya Uyui na kwamba walilengwa vijana 210 lakini waliofika
na kupata mafunzo hayo ni vijana 191.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui
Said Ntahondi amemuomba mkuu huyo wa mkoa kuyataka makampuni yanayonunua zao la
tumbaku mkoani Tabora kuwatumia vijana hao kupanda miti na shughuli nyingine
zinazotokana na zao hilo badala ya kuchukua watu wengine.
No comments:
Post a Comment