Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Sunday, January 3, 2016

WAWILI KIZIMBANI KWA KUGHUSHI, KUTUMIA MADARAKA VIBAYA.



Na, Thomas  Murugwa, Tabora.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imewafikisha mahakamani watu wawili kwa tuhuma tofauti  mmoja kwa kuhujumu uchumi  na mwingine kughushi nyaraka hivyo wote  kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Waliofikishwa mahakamani  ni aliyekuwa afisa misitu  msaidizi wa wilaya ya Sikonge  Krety John ambaye anakabiliwa na mashtaka saba ya kutumia madaraka vibaya na Cathberth Ndogoma aliyekuwa mratibu wa  Tabora NGOS Cluster  akiwa na tuhuma 19 za kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri.

Katika kesi inayomkabili  Krety John ilidaiwa na wakili wa TAKUKURU Edson Mapalala mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Tabora Emanuel Ngigwana kuwa alitenda makosa hayo kati ya  tarehe 26 Machi 2010 na tarehe 25,2012 huko wilaya ya Sikonge na kumsababishia mwajiri hasara ya zaidi ya shilingi milioni  27.

Wakili Mapalala aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa akiwa mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge kama afisa misitu msaidizi alitoa vibali vya kusafirishia mazao ya misitu kwa watu mbali mbali bila kuzingatia sheria ya misitu.

Wakili huyo alibainisha kuwa mnamo tarehe 26 Machi 2010 mtuhumiwa kwa makusudi alitoa kibali chenye thamani ya shilingi milioni tatu na kati ya tarehe 12 Julai na tarehe 16 Oktoba 2010 alitoa vibali vyenye thamani ya shilingi 10,052,800/- bila kuzingatia  sheria ya misitu.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa mtuhumiwa akiwa ni mtumishi wa serikali kati ya desemba 16/2010 na machi mosi 2012 alitumia madaraka yake vibaya kwa  kutoa vibali  vyenye thamani ya shilingi milioni  14,004,000/= na kuisababishia hasara serikali.

Ilidaiwa  kwenye shitaka la saba kuwa kati ya machi 2010 na machi 2/2012 mtuhumiwa alishindwa kutimiza majukumu yake na kuisababishia serikali hasara  ya shilingi milioni 27,666,400/=.

Mtuhumiwa huyo yupo nje kwa dhamana hadi januari 11 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

Katika kesi inayomkabili Kathberth Ndogoma ilidaiwa na wakili huyo wa TAKUKURU mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Tabora Joctan Rushwela kuwa alitenda makosa hayo kati  ya tarehe 11 Novemba 2008 na tarehe 23 Disemba 2008 akiwa mfanyakazi wa taasisi ya Tabora NGOs Cluster.

Wakili Mapalala alidai kuwa katika kipindi hicho na kwa tarehe tofauti mtuhumiwa kwa lendo la kudanganya alighushi daftari la mahudhurio  likionyesha majina ya watu walihudhuria mafunzo ya utoaji huduma kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na ukimwi majumbani.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa pia alighushi hati mbali mbali za malipo zikionyesha kwamba amewalipa watu waliohudhuria mafunzo hayo kiasi cha shilingi elfu tano kila mmoja hivyo kuisababishia hasara Tume ya kudhibiti UKIMWI nchini TACAIDS ambayo ilitoa fedha hizo.

Mapalala alidai kuwa mtuhumiwa kwa makusudi alibadili matumizi ya fedha na kusababisha hasara  ya  shilingi milioni 6,496,000/- zilizotolewa na TACAIDS  kwa ajili ya mafunzo  ya wanaowahudumia wanaoishi na Virusi vya UKIMWI majumbani . 

Mtuhumiwa alikana tuhuma zote 19 lakini wadhamini wake walishindwa kutimiza masharti ya dhamana alipelekwa rumande hadi januari 14 mwaka kesi yake itakapoanza usikilizwaji wa awali.

Saturday, January 2, 2016

KUMCHAYA:MKAPA NI KIOO CHA WAANDISHI WA HABARI KUONGEZA MAARIFA NA UFAHAMU



Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa

Na Paul Christian, Tabora.

Waandishi wa habari mkoani Tabora wameaswa kuongeza maarifa na ufahamu kwa kusoma vitabu na machapisho mbalimbali ili kuongeza tija katika kazi zao za kuhabarisha, kujulisha na kuburudisha.

Mkuu wa wilaya ya Tabora Suleiman Kumchaya amesema hayo alipokua akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika kuutathimini mwaka 2016 na tasnia hiyo.

Amesema, “Kusoma sana kunaongeza uwezo wa kufahamu na kuchambua mambo mbalimbali kwa kina, hali hii itawafanya waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyosasa.”

Mkuu huyo wa wilaya amehimiza waandishi hao kutopuuza suala la kusoma kwa kuwa mwaka 2016 utakuwa wa mabadiliko katika Nyanja za kiuchumi,kisiasa,kijamii na kiutamaduni na kwamba uchambuzi yakinifu wa waandishi hao utasaidia kuharakisha mabadiliko hayo.

Kumchaya amewataka waandishi hao kuiga mfano wa Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa ambaye muda wake mwingi anautumia kusoma vitabu na machapisho mbalimbali hata wakati akiwa Rais wa nchi.

“Mzee Mkapa akiwa kiongozi wa nchi hakupenda vitu vya anasa hata anapokuwa nje ya nchi muda mwingi aliutumia kusoma vitabu.” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Kumchaya ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Rais huyo wa awamu ya tatu amesema, “ukitaka kuelewana na mzee Mkapa mwambie nimeona kitabu kizuri mahali fulani na sio viatu vizuri au vitu vya anasa.”

Suleiman Kumchaya amewahi kufanyakazi kwenye shirika la utangazaji Tanzania TBC zamani likijulikana kama Radio Tanzania na idhaa zake mbalimbali.
Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa ni mwandishi wa habari na amewahi kuwa mwandishi wa Rais wa awamu ya kwanza Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

SEHEMU YA KWANZA:TUNAJIFUNZA NINI KWA TUKIO HILI LA KIHISTORIA



                                      OPERESHENI ENTEBBE


Paul Christian, Tabora.

Ilikuwa majira ya saa tano usiku wa tarehe 3 Julai 1976 makomandoo wapatao 100 wa jeshi la Israel (IDF) walivamia uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Entebbe nchini Uganda na kuwakomboa mateka wenye asili ya Israel waliokuwa wakishikiliwa kwenye moja ya majengo ya uwanja huo.

Uvamizi huo wa  jeshi la Israel ulipewa jina la  Operesheni Entebbe au Thunderbolt au Yonatan “Jonathan” kwa kumbukumbu ya luten Kanali Yonatan Netanyahu askari pekee wa Isarel aliyeuawa kwenye operation hiyo.

Wiki moja kabla ya operesheni hiyo tarehe 27 Juni, 1976 ndege ya abiria Air  France 139, aina ya  Airbus A300B4-203, yenye namba za usajili F-BVGG (c/n 019),  ilikuwa ikisafiri kutoka Ben Gurion,Israel kuelekea Charles De Gaulle,Ufaransa kupitia Ellinikon,Ugiriki ilitekwa nyara. 

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 248 na wafanyakazi 12 ilitekwa nyara na wapiganaji wa kundi la ukombozi wa wapalestina yaani  Popular Front for the Liberation of Palestine – External Operations (PFLP-EO)  kwa amri ya  kiongozi wa kundi hilo Wadie Haddad

Kundi hilo la PFLP-OE lilijitenga kutoka  kundi mama la Popula Front for the Liberation of Palestine PFLP lililokuwa likiongozwa na George Habash.

Ndege hiyo ilitekwa Nyara na wapiganaji hao baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa Ellinikon  jijini Athens, Ugiriki ambapo abiria 58 wakiwemo wateka nyara wanne walipanda.

Mara baada ya kuondoka kwenye uwanja huo wateka nyara hao waliibuka na kuwataka marubani kuiongoza ndege hiyo kuelekea Benghazi Nchini Libya ambapo ilikaa kwa saa saba kwa ajili ya kuongeza mafuta.

 Ndege hiyo ikiwa Benghazi,  watekaji hao walimwachia huru mateka mmoja mzaliwa wa uingereza mwenye uraia wa Israel Patricia Martell ambaye alijifanya ameharibu ujauzito wake kwa mshituko.
 
Hatimaye Ndege hiyo ya Air France 139 iliondoka Benghazi na kutua  kwenye uwanja wa ndege wa kimaitaifa wa Entebbe nchini Uganda majira ya saa 9 na dakika 15 Alasiri siku ya tarehe 28 Juni, 1976. 

Rais wa Uganda Idd Amin binafsi aliwaunga mkono watekaji hao na kuwakaribisha kwenye ardhi ya Uganda.Aliwatembelea mara kwa mara na kuwaambia mateka hatua za mazungumzo ili waachiwe huru.

Mnamo tarehe 28 Juni, 1976  Wateka Nyara hao wanne ambao wawili wakiwa wapalestina na wengine wawili wakiwa wajerumani wanachama wa kundi la German Revolutinary Cells, walitoa madai yao kwa serikali ya Israel.

Katika madai yao watekaji hao walitaka kuachiliwa huru wafungwa 40 wakiwemo wanamgambo wa kipalestina waliofungwa kwenye magereza ya nchini Israel.

Pili, walitaka kuachiwa huru kwa wafungwa wengine 13 waliofungwa kwenye magereza ya mataifa mengine manne.

Tatu,walitaka kulipwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 5 kwa ajili ya kuiachia huru ndege hiyo ya Air France 139 na kwamba madai hayo yalipaswa kutekelezwa hadi kufikia tarehe 1 Julai, 1976. 

Ndege hiyo ilipotua kwenye uwanja huo wa Entebbe huku ikilindwa na askari wa jeshi la Uganda, abiria pamoja na wafanyakazi wote wa ndege hiyo waliamriwa kushuka na kisha kupelekwa kwenye jengo la zamani lisilotumiwa kwa shughuli za abiria.

Mnamo tarehe 29 Juni, 1976 abiria mateka walitengwa makundi mawili baada ya jeshi la Uganda UDF kubomoa ukuta uliokuwa ukiwatenganisha chumba cha mapokezi na chumba kingine katika jengo hilo.

Watekaji waliwachambua na kuwatenga raia wa Israel wakiwemo raia wa Israel wenye uraia wa nchi mbili kutoka kwa raia wa nchi nyingine miongoni mwa mateka hao, na raia hao wa Israel waliamriwa kuingia kwenye chumba kimoja. 

Aidha mateka wasio kuwa raia wa Israel waumini wa madhehebu ya Orthodox wanandoa wanne kutoka Marekani na Ubelgiji, na Mfaransa mkazi wa Israel waliunganishwa kwenye kundi lililotengwa la waisrael.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mmoja wa mateka hao watano mfaransa Monique Epstein Khalepski alisema walichukuliwa na watekaji kwa ajili ya mahojiano kwa kuwahofiwa kuficha utambulisho wa uraia wao.

Naye Mateka Mfaransa Michel Cojot-Goldberg alisema watekaji walishindwa kumtambua muisrael mateka aliyekuwa afisa wa jeshi mwenye uraia wa nchi mbili baada ya kuonesha paspoti isiyokuwa ya Israel na baadae aliondoka na kundi la pili la mateka walioachiwa huru.

Raia wa Marekani Janet Almog, Mwanamke Mfaransa Jocelyne Monier ambaye mwenzi wake alikuwa muisrael, na Jean-Jacques Mimouni mwenye uraia wa nchi za Ufaransa na Israel ambaye jina lake halikuitwa kwenye orodha ya majina ya abiria, walichagua kwa hiari zao kujiunga na kundi la mateka wa Israel.

Tarehe 30 Juni, 1976  watekaji waliwaachia huru mateka 48 kutoka kwenye kundi la mateka wasiokuwa raia wa Waisrael ambao wengi wao walikuwa wazee, wagonjwa, wakinamama na watoto. 

Mateka 47 kati yao walisafirishwa kueleka Paris, Ufaransa, na abiria mmoja Dora Bloch mwenye umri wa miaka 75 alipelekwa hospitali nchini Uganda kutokana na hali yake ya afya kuwa mbaya.

Tarehe 1 Julai, 1976 ilikuwa siku ya mwisho iliyotolewa na watekaji hao ili madai yao yatekelezwe, serikali ya Israel ilikubali kufanya mazungumzo kuhusu madai ya watekaji.

Kutokana hali hiyo watekaji wakaongeza siku za mazungumzo na kwamba siku ya mwisho ya utekelezaji wa madai yao ikawa majira ya mchana ya tarehe 4 Julai, 1976.

CHAMA CHA WANANCHI CUF: MAGUFULI ANATEKELEZA SERA ZA UKAWA


Rais wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli

 Na Hastin Liumba,Kaliua

CHAMA cha wananchi (CUF) wilaya ya Kaliua mkoani Tabora kimempongeza Rais John Magufuli kwa  kutekeleza sera za upinzani.

Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kaliua Lubaga Katwiga alisema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari wilayani humo.

Katwiga alisema hatua anazochukua Rais Magufuli kwa sasa zilikuwa ni sehemu ya sera na ilani ya vyama vilivyokuwa vinaunda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA.

 Alisema endapo UKAWA ungeshinda uchaguzi wa Oktoba 25,2015 hayo anayoyafanya Magufuli yangetekelezwa na wao ikiwa ni sehemu ya kushughulikia kero za wananchi.

Aidha mwenyekiti huyo alichukua nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wa jimbo la Kaliua kwa kumchagua mbunge toka chama cha wananchi CUF Magdalena Sakaya.

Katwiga alisema mbunge huyo ni chaguo sahihi kwa wanakaliua kwani ni mtu makini na mfuatiliaji wa kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Mwenyekiti huyo wa CUF alisisitiza kuwa wananchi wa jimbo hilo watarajie mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii chini ya uongozi wa mbunge huyo na kwamba hawatajuta kumchagua.





KATIKA HISTORIA:KITI ALICHOTUMIA MBUNGE WA TABORA MJINI 2005-2010

Kiti kilichotumiwa na Siraju Kaboyonga
Hiki ni kiti kilichotumiwa na Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Siraju Juma Kaboyonga (2005-2010) kwenye ofisi yake iliyokuwa kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya ya Tabora. 

Mbunge huyo alizaliwa tarehe 31 Agosti,1949 na kufariki dunia tarehe 11 Disemba,2012 jijini Dar es Salaam.

Atakumbukwa kwa sera zake za uwazi na ukweli kwa wapiga kura wake hakupenda kumung'unya maneno na kuingiza siasa za uongo pale anapokutana na jambo.



Hili ni Gofu la jengo lililotumika kama hospitali ya kutibu wazungu na Mapadri wakati wa utawala wa Wajerumani, Jengo hili lipo barabara ya shule jirani na ofisi za chuo cha VETA Kanda ya Magharibi mjini Tabora.