Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, July 9, 2016

VIONGOZI WATANO WA KIJIJI WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UHUJUMU UCHUMIUCHUMI




 Na Thomas Murugwa,Igunga.

Viongozi watano wa  serikali ya kijiji cha Igogo wilaya ya Igunga  mkoani Tabora wamefikishwa mahakama ya Wilaya hiyo wakikabiliwa na mashitaka manne ya kuhujumu uchumi.

Viongozi hao waliopandishwa kizimbani ni mwenyekiti wa kijiji hicho Elinkaila Issa, afisa mtendaji Henry Luhende Masanja, wajumbe wa kamati ya fedha Helena Maduluma  na Boniphace Jagadi pamoja  na mtunza hazina Emanuel Simon.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Edsoni Mapalala wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  TAKUKURU ulidai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Igunga Ajali Milanzi kuwa watuhumiwa walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 13 na Novemba 24, 2014.

Katika shitaka la kwanza ilidaiwa kuwa tarehe 13 Oktoba 2014 watuhumiwa kwa kutumia nyadhifa zao waliiba shilingi 5,100,000/- fedha za shule ya msingi Igogo.

Wakili mapalala alisema kuwa watuhumiwa kwa kutumia nyadhifa zao vibaya waliiba kiasi hicho cha fedha ambazo zilikuwa zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa matundu 12 ya vyoo vya shule ya msingi Igogo.

 Ilidaiwa katika shitaka la pili na wakili Mapalala kuwa tarehe 24 Novemba 2014 watuhumiwa kwa pamoja waliiba shilingi 3,120,00/- zilizokuwa  zimetolewa  kwa  ajili  ya ujenzi wa choo cha ofisi ya serikali ya kijiji hicho. 

Katika shitaka la tatu  ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa watuhumiwa kwa pamoja na kwa makusudi  wakiwa  viongozi wa kamati ya fedha ya serikali ya kijiji hicho walijitwalia jumla ya shilingi 8,220,000/- na kusababisha ujenzi wa matundu ya vyoo kutojengwa.

Wakili Mapalala alidai katika shitaka la nne kuwa kutokana na kitendo hicho  watuhumiwa waliisababishia halmashauri ya wilaya ya Igunga hasara ya shilingi 8,220,000/=.

Watuhumiwa wote wamekana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana hadi julai 12 mwaka huu shauri hilo litakapoanza usikilizwaji wa awali kwani upelelezi wake umekamilika.

Friday, July 1, 2016

MWANRI:AZIGIZA HALMASHAURI KUTENGA ASILIMIA TANO YA MAPATO YA NDANI KWA AJILI YA VIJANA



Na Paul Christian,Tabora

Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani Tabora zimeagizwa kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha vijana katika maeneo yao.

Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa agizo hilo jana alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya kutambua fursa za ajira kwa vijana 191 wa wilaya ya Uyui yaliyofanyika katika chuo cha kilimo Tumbi katika manispaa ya Tabora.

“Ninaanza kucheck mahesabu ya halmashauri zote za mkoa wa Tabora na nikibaini halmashauri ambayo haijatenga asilimia tano kwa ajili ya vijana hatutapitisha bajeti ya halmashauri husika,” amesema.

Mwanri amesisitiza kuwa suala la kutenga asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauri hizo ni la kisheria na kwamba halina mjadala.

Aidha amezitaka halmashauri hizo kuweka vipaumbele madhubuti katika mipango yao ili ziweze kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwakwamisha vijana kujichukulia fursa mbalimbali za kiuchumi.

“Halmashauri zinapaswa kuweka vipaumbele katika kuchimba mabwawa, kutengeneza miundombinu ya barabara pamoja na mambo mengine kwa lengo la kuwafanya vijana wanaojiajiri wayafikie masoko na kutoa huduma mbalimbali za kibiashara.”Amesema Mwanri.

Mkuu huyo wa mkoa amezitaka halmashauri hizo kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana ili wawe wabunifu wa kujiajiri na kutoa ajira kwa watu wengine.

Akitoa rai kwa vijana hao amesema wanapaswa kubadili mtazamo wa kutaka kuajiriwa na badala yake wafikirie kuwa waajiri wa wale wanaofikiria kuhitimu masomo na kuajiriwa.

Awali kiongozi wa shirika la Millenium Promise Tanzania Dkt. Gerson Nyadzi amesema mafunzo hayo yanatokana na mradi unaojulikana Opportunities for Youth Employment (OYE).

“Vijana hawa wamejifunza nini maana ya mawasiliano,kuwa na nia au malengo katika maisha yao,kuweka kumbukumbu na kuhesabu,namna ya kupunguza msongo (stress management) pamoja na mawasiliano na utambuzi wa fursa.” Amesema.

Amesema mafunzo hayo ni ya awali yanayojulikana kama “stadi za kijamii” na hatua itakayofuata itakuwa ni kufundishwa masuala ya utaalam au ufundi (technical skills training).

Nyadzi amebainisha kuwa katika mafunzo hayo ya awali vijana hao wamejifunza kwa kujigawa katika makundi makuu matatu ikiwemo kilimo cha bustani,ufugaji wa kuku na nyuki.

Ameyataja makundi mengine kuwa ni kutafuta nishati mbadala (renewable energy) ambapo watafanya biogas na utengenezaji wa majiko banifu pamoja na kundi la usafi wa mazingira na maji ( water sanitation and hygiene).

Dkt. Nyadzi amesema vijana hao wenye umri wa kati ya miaka 18 na 30 wanatoka katika kata za Magiri,Ilolangulu,Kigwa,Isila na Isikizya katika wilaya ya Uyui na kwamba walilengwa vijana 210 lakini waliofika na kupata mafunzo hayo ni vijana 191.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Said Ntahondi amemuomba mkuu huyo wa mkoa kuyataka makampuni yanayonunua zao la tumbaku mkoani Tabora kuwatumia vijana hao kupanda miti na shughuli nyingine zinazotokana na zao hilo badala ya kuchukua watu wengine.



Saturday, June 4, 2016

MSTAAFU ALIA NA HALMASHAURI YA MANISPAA YA TABORA KUSHINDWA KUMLIPA MAPUNJO YAKE



Na Mwandishi Wetu,Tabora

MSTAAFU aliyekuwa mtumishi wa halmashauri ya Manispaa Tabora Daud
Timotheo (70) amelia na uongozi halmashauri hiyo kushindwa kumlipa
haki yake kama mapunjo ya mshahara kiasi cha shilingi milioni 1.3.

Akiongea na waandishi wa habari mstaafu huyo amesema amefuatilia madai yake kwa muda mrefu bila mafanikio hali ambayo imemlazimu kueleza kilio chake hadharani ili asaidiwe kupata haki yake.

Timotheo amesema alistaafu  mwaka 2013 akiwa mhudumu idara ya afya katika halmashauri ya manispaa hiyo na kwamba amepunjwa muda wa miezi 15 kwa kulipwa mshahara pungufu.

Amebainisha kuwa hadi anastaafu mapunjo ya mshahara wake yalikuwa ni jumla ya shilingi milioni 1,392,710.00.

Anasema alikuwa analipwa mshahara wake kwa mwezi shilingi 255,050 kuanzia mwezi Januari 2009 hadi mwezi Novemba 2009.

Aidha ameongeza kuwa katika kipindi hicho  alikuwa akipokea mshahara wa shilingi  128,410.00 ukiwa ni pungufu ya mshahara halisi wa  shilingi 255,050.00

Timotheo amebainisha kuwa hata hivyo alirekebishiwa mshahara wake ambapo mwezi Disemba 2009 alianza kulipwa mshahara wake kamili wa shilingi 255,050.00 lakini mapunjo yake hadi leo hajalipwa na mwajiri wake huyo.

Amesema amechoshwa na hali hiyo ya kuzungushwa kulipwa fedha zake za mapunjo kwa kuwa inamkwamisha kufanya shughuli nyingine ya kujiongezea kipato.

Timotheo anasema amendika barua ya kulalamika ya mwezi Machi 27,mwaka 2010 na kuambatanisha vielelezo vyote (Salary Slip) ya miezi Disemba 2008,Januari 2009 na Disemba 2009.

Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Tabora Sipola Liana akizungumzia suala hilo amesema kuwa amemuagiza mkaguzi wa ndani kuhakiki deni hilo na taratibu ziandaliwe ili haki ya mstaafu huyo zipatikane.



MWANRI: AAGIZA MGOGORO WA KIWANJA CHA TBC UMALIZWE NDANI YA WIKI TATU



Na Hastin Liumba,Tabora

MKUU wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa wiki tatu kwa mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa Tabora Sipola Liana kuhakikisha mgogoro wa kiwanja kati ya shirika la utangazaji Tanzania TBC, halmashauri hiyo na wananchi unapatiwa utatuzi.

Agizo hilo amelitoa kwenye kikao cha maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo wakati wa kuchangia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Mkuu huyo wa mkoa amesema amefuatilia nyaraka za TBC na kugundua kiwanja hicho ni mali ya shirika hilo, hivyo wananchi wanaoendelea kujenga katika kiwanja hicho ni wavamizi na waondolewe.

"Natoa wiki tatu kwako mkurugenzi kuhakikisha mgogoro wa kiwanja cha TBC unamalizwa na nipewe taarifa kabla ya kuchukua hatua."alisisitiza.

Mwanri amesema jambo hilo liko wazi lakini anashangazwa na uongozi wa manispaa kushindwa kuchukua hatua.

"Nilichogundua kuna udhaifu wa kiuongozi na idara ya ardhi kuna ubabaishaji wa hali ya juu, ni lazima tuchukue hatua dhidi ya wahusika."ameonya.

Amefafanua haiwezekani kiwanja kimoja kinatolewa kwa watu wawili na kupelekea mgogoro baina yao.

Amesema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakimueleza Manispaa Tabora kushindwa kumaliza matatizo hayo.

Amesema yeye ni mwakilishiwa Rais hivyo asingependa kuona katika mkoa wake watendaji wanaofanya kazi kwa mazoea na kwamba wanaacha mara moja.

Katika hatua nyingine baraza la madiwani la manispaa hiyo lilipitisha azimio la kuwasimamisha kazi watumishi wanne wa idara ya ardhi ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma mbalimbali zinazoikabili idara hiyo.

Watumishi hao waliosimamishwa ni Mohammed Matola,Stanley Yungi,Lazaro Iragila na Allan Mbato ambao wanatuhumiwa na wananchi katika suala zima la viwanja manispaa Tabora.

Hatua hiyo ni ya pili kuchukuliwa na baraza hilo la madiwani ambapo kwa mara ya kwanza iliwasimamisha kazi watumishi watano wa idara hiyo lakini walirejeshwa kazini mamlaka za juu za serikali.

SARATANI YA NGOZI TISHIO KWA MAISHA YA ALBINO.



Na,Thomas Murugwa, Tabora.

Serikali ya awamu ya Tano imetakiwa za kunusuru maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi vinavyotokana na ugonjwa wa saratani ya ngozi.
 
Uchunguzi uliofanywa na blog hii umebaini kuwa vifo 10 vya watu wenye ulemavu wa ngozi  vimetokea kati ya Januari na Mei 2016  mkoani Tabora kutokana na ugonjwa huo kwa kukosa mafuta maalumu  yanayosaidia kupunguza mionzi ya jua kuifikia ngozi ya watu hao.

Katibu wa chama cha Maalbino mkoani Tabora Ramadhani Nassoro amesema  saratani ya ngozi imesababisha vifo hivyo na hiyo imekuwa ni  changamoto kwao kwa kuwa  inachangia kufupisha maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Amesema kuwa watu wanye ulemavu wa ngozi wengi wao maisha yao hayazidi miaka (40) kwa kuwa wanakabiliwa na hatari ya saratani ya ngozi ambayo inatokana na kufikiwa na mionzi ya jua moja kwa moja.

Nassoro amebainisha kuwa albino wanakutana na mionzi ya jua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufanya kazi za kujipatia kipato kama kilimo, uchungaji,ujenzi na nyingine katika maeneo ya wazi.

Naye Juma Mosha katibu wa chama cha Albino wilaya ya Nzega mkoani Tabora ameiomba serikali ichukue jukumu la kuwapatia mafuta hayo maalumu kupitia  hospitali na vituo vya afya ili kuwanusuru na saratani ya ngozi ambayo inakatisha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Katibu huyo amebainisha kuwa mafuta hayo yanagharama kubwa hali ambayo albino wengi hawawezi kumudu na kwamba wakati umefika kwa serikali kuwasaidia kama ambavyo imeamua kufanya hivyo kwa wazee.